Kipa wa timu ya taifa ya Hispania, Misa Rodríguez, amejiunga na klabu ya Arsenal Women kwa uhamisho wa bure (free transfer) baada ya kumaliza safari yake ya miaka sita akiwa na Real Madrid.
Arsenal ilithibitisha usajili huo Jumatano, Julai 22, 2026, huku Rodríguez akieleza furaha yake ya kuanza changamoto mpya katika maisha yake ya soka.
“Nina furaha sana kuwa sehemu ya timu hii na kukabiliana na changamoto mpya. Nataka kusaidia timu kushindania mataji,” alisema Rodríguez.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alikuwa nahodha wa Real Madrid msimu uliopita na amecheza jumla ya mechi 215 akiwa na klabu hiyo kwa kipindi cha misimu sita.
Kwa upande wa timu ya taifa, Rodríguez ameichezea Hispania mara 24 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa Kombe la Dunia la Wanawake 2023 pamoja na UEFA Women’s Nations League 2024.
Arsenal Women, waliomaliza nafasi ya pili nyuma ya Manchester City msimu uliopita, wataanza kampeni yao ya Ligi Kuu ya Wanawake England (WSL) mwezi Septemba.