Nyota wa Hispania, Lamine Yamal, alisherehekea ushindi wa kihistoria wa timu yake kwa namna ya kipekee baada ya kumkumbatia mdogo wake wa miaka mitatu, Keyne, mara tu baada ya Hispania kuibuka mabingwa wa Kombe la Dunia 2026 kwa kuifunga Argentina mabao 1-0.
Baada ya filimbi ya mwisho katika fainali iliyochezwa Julai 19, 2026, Keyne alionekana akikimbia kwa furaha kuelekea uwanjani akiwa amevaa jezi nyekundu ya Hispania. Video iliyosambaa mitandaoni ilimuonyesha mtoto huyo akimkimbilia kaka yake na kuruka mikononi mwake huku wakikumbatiana kwa furaha kubwa.
Keyne alikuwa ameshika kipande cha wavu wa goli kama kumbukumbu ya ushindi huo, huku Yamal akimbeba na kumkumbatia mbele ya mashabiki waliokuwa wakishangilia ushindi wa Hispania.
Keyne ni mmoja wa ndugu wa kambo wa Yamal pamoja na dada yake, Baraa. Ni mtoto wa mama yake Yamal, Sheila Ebana, ambaye alimzaa Keyne mwaka 2022 baada ya kuolewa tena kufuatia kuachana na baba wa Yamal, Mounir Nasraoui.
Uhusiano wa karibu kati ya Yamal na mdogo wake umeendelea kuwavutia mashabiki tangu mshambuliaji huyo aanze kung’ara akiwa Barcelona mwaka 2023. Katika safari ya Hispania kuelekea ubingwa wa dunia, Keyne alionekana mara kadhaa akimshangilia kaka yake, ikiwemo baada ya ushindi dhidi ya Ufaransa kwenye nusu fainali, ambapo pia alimkimbilia na kumkumbatia kwa furaha.
Hispania ilitwaa taji lake la kwanza la Kombe la Dunia tangu mwaka 2010 baada ya kuifunga Argentina 1-0 kupitia bao la mshambuliaji Ferran Torres dakika ya 106 ya muda wa nyongeza.
Fainali hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Yamal kushiriki Kombe la Dunia, huku akitoa mchango mkubwa katika safari ya Hispania ya kutwaa ubingwa na kuandika historia mpya ya soka la taifa hilo.