FIFA Yashutumu UEFA Kwa “Kampeni ya Upotoshaji” Dhidi ya Infantino

FIFA imeishutumu UEFA kwa kuendesha kile ilichokiita “kampeni ya upotoshaji” pamoja na kujaribu kuathiri uchaguzi wa urais wa FIFA, huku ikiomba Mahakama ya Marekani ikatae ombi la UEFA la kupata nyaraka na ushahidi kutoka kwa taasisi hiyo.

UEFA mwezi uliopita iliwasilisha ombi katika Mahakama ya Shirikisho nchini Marekani ikitaka ruhusa ya kupata ushahidi na nyaraka zitakazotumika katika malalamiko ya jinai yanayopangwa kuwasilishwa nchini Uswisi dhidi ya Rais wa FIFA, Gianni Infantino.

Malalamiko hayo yanahusishwa na mpango uliokuwa umepewa jina la FIFA Forward Enterprise (FFE), ambao ulikuwa na lengo la kuhamisha baadhi ya haki za kibiashara za Kombe la Dunia kwenda katika kampuni hiyo. Mpango huo ulisitishwa mwezi Julai baada ya kukabiliwa na upinzani kutoka kwa mashirikisho mbalimbali, yakiwemo UEFA, CONCACAF na Shirikisho la Soka la Asia.

Katika majibu yake yaliyowasilishwa Jumatatu, FIFA ilidai kuwa nyaraka za UEFA zina “taarifa nyingi za uongo au zinazopotosha” kuhusu FIFA na Infantino.

FIFA pia imekanusha madai kwamba Infantino alikusudia kujinufaisha binafsi kupitia mpango wa FFE, ikisema mpango huo ulipaswa kupata idhini kutoka kwa vyama wanachama wa FIFA pamoja na Baraza la FIFA.

Mzozo Kuhusu Thamani ya FFE

UEFA ilidai kuwa wawekezaji walikuwa tayari kulipa dola bilioni 4.2 kwa hisa katika FIFA Forward Enterprise, jambo ambalo lingeifanya kampuni hiyo kuwa na thamani ya takribani dola bilioni 20.

UEFA ilisema thamani hiyo ilidharau kwa kiasi kikubwa haki za kibiashara za FIFA na kwamba mchakato huo haukuhusisha zabuni ya wazi wala tathmini huru.

Hata hivyo, FIFA imekanusha hoja hiyo, ikisema UEFA imechanganya “equity value” na “enterprise value.”

Kwa mujibu wa FIFA, thamani ya hisa ya FFE ilikuwa dola bilioni 20, huku thamani ya jumla ya biashara ikiwa zaidi ya dola bilioni 30.

Mzozo Wafikia Uchaguzi wa Urais FIFA

FIFA pia imedai kuwa hatua za kisheria zinazochukuliwa na UEFA zinaweza kuwa na uhusiano na uchaguzi wa urais wa FIFA unaotarajiwa kufanyika Machi 2027, ambapo Infantino anawania kuchaguliwa tena.

Wiki iliyopita, Infantino aliwaandikia vyama vyote 211 wanachama wa FIFA akipendekeza kufanyika kwa mapitio huru ya mifumo ya maamuzi na utawala wa taasisi hiyo.

FIFA imesema hatua ya UEFA ya kuwasilisha nyaraka hizo mahakamani wakati uchaguzi huo ukikaribia ni jaribio la kuathiri uchaguzi huo.

UEFA haikuwa imetoa majibu mara moja kwa ombi la Reuters la kutoa maoni kuhusu tuhuma hizo.