ABUJA, NIGERIA: Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limetangaza kuwa vyama vyote 54 vya soka vya nchi wanachama vimekubaliana kumuunga mkono Gianni Infantino katika uchaguzi ujao wa urais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Msimamo huo umetangazwa na Rais wa CAF, Patrice Motsepe, wakati wa Mkutano Mkuu wa 48 wa shirikisho hilo uliofanyika jijini Abuja, Nigeria.
Motsepe amesema vyama vyote 54 vya soka barani Afrika vimewasilisha nyaraka rasmi kuthibitisha uungwaji mkono wao kwa Infantino, ambaye anawania kuendelea kuiongoza FIFA kwa muhula wa nne.
Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Machi 18, 2027, jijini Rabat, nchini Morocco.
Infantino alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Rais wa FIFA mwaka 2016, akichukua nafasi ya Sepp Blatter, na tangu wakati huo amekuwa akiongoza chombo hicho kinachosimamia soka duniani.
Uamuzi wa vyama vya soka vya Afrika kuwasilisha uungwaji mkono wao kwa Infantino unaweka wazi msimamo wa pamoja wa bara hilo kuelekea uchaguzi huo, huku macho ya wadau wa soka yakielekezwa Morocco ambako uchaguzi huo utafanyika.
Kwa hatua hiyo, Afrika imewasilisha msimamo wake kupitia CAF, huku Infantino akiendelea na jitihada za kutafuta muhula mwingine wa kuongoza FIFA.