DAR ES SALAAM, Septemba 24, 2026 — Serikali ya Tanzania imelipa Dola za Marekani milioni 32, sawa na takriban Shilingi bilioni 74, kwa ajili ya kupata uenyeji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda, amesema hayo leo, Septemba 24, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu uwekezaji wa Serikali katika sekta ya michezo na usimamizi wa nembo za taifa.
Kwa mujibu wa Makonda, fedha hizo ni sehemu ya gharama za kuipatia Tanzania uhalali wa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, na si fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanja, barabara au miundombinu mingine.
“Tumelipa sisi taifa kuwa wenyeji wa AFCON milioni 32, sawa na takriban bilioni 74. Hii ni pesa ya kuwa tu mwenyeji,” amesema Makonda.
Tanzania yazungumza na CAF kuhusu haki za matangazo
Makonda amesema Serikali pia ipo katika mazungumzo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuhusu malipo ya Dola za Marekani milioni 12, sawa na takriban Shilingi bilioni 30, kwa ajili ya kupata haki za matangazo ya televisheni za AFCON 2027.
Amesema uwekezaji huo unaangaliwa kwa mtazamo mpana zaidi ya michezo, ikiwemo kuitangaza Tanzania kimataifa, kukuza utalii na kuvutia wawekezaji.
“Fedha hizi sio za kujenga uwanja, sio za kununua maji, sio za kujenga barabara. Kama nchi tumelipa ili tupate uhalali wa ku-host haya mashindano,” amesema.
Ameongeza kuwa Tanzania inatarajia kutumia fursa ya mashindano hayo kuitangaza nchi na kuonyesha fursa zilizopo kwa wageni na wawekezaji watakaofika nchini.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, uwekezaji huo pia unalenga kuchochea shughuli za kiuchumi na kusaidia kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Jezi ya Taifa Stars nayo yatajwa
Akizungumzia suala la jezi ya Taifa Stars, Makonda amesema kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuiwakilisha Tanzania kwenye jukwaa la kimataifa, jezi ya timu hiyo inapaswa kupewa thamani na uzito unaostahili.
Amesema jezi ya Taifa Stars ni miongoni mwa alama zinazotambulisha Tanzania na hivyo suala la uzalishaji, utambulishaji na uuzaji wake linapaswa kufanyika kwa utaratibu rasmi.
Makonda amesisitiza kuwa jezi hiyo haipaswi kuchukuliwa kama bidhaa ya kawaida, bali inapaswa kuangaliwa pia kama sehemu ya nembo ya taifa na fursa ya kuitangaza Tanzania.
Kauli hiyo imekuja wakati Tanzania ikiendelea na maandalizi ya AFCON 2027, ambayo inatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa ya michezo yatakayoiweka nchi katika uangalizi wa kimataifa.