DAR ES SALAAM, Septemba 24, 2026 — Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema jezi ya Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ni sehemu ya utambulisho na nembo ya nchi, hivyo haipaswi kuzinduliwa au kutangazwa bila kushirikisha mamlaka husika.
Makonda ameyasema hayo leo, Septemba 24, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akisisitiza kuwa Taifa Stars ni mali ya nchi na si mali ya mtu binafsi wala kampuni.
Amesema kwa kuwa timu hiyo inaiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa, hatua muhimu zinazohusu timu hiyo zinapaswa kufanyika kwa utaratibu unaotambuliwa na mamlaka husika.
“Timau ya Taifa ni mali ya nchi, si ya mtu binafsi wala kampuni,” amesema Makonda, akisisitiza kuwa hata suala la jezi linapaswa kupewa uzito unaostahili kwa sababu linahusisha utambulisho wa taifa.

Wizara yataka kushirikishwa
Makonda amesema mamlaka ya Wizara yanaanzia katika sera, miongozo na kanuni, huku usimamizi wa Taifa Stars ukiwa umekasimishwa kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Hata hivyo, amesema kwa kuwa Taifa Stars ni timu inayoiwakilisha nchi, Waziri anapaswa kufahamu hatua muhimu zinazohusu timu hiyo.
Ameeleza kuwa tangu Februari mwaka huu kulikuwa na vikao vilivyohusu maandalizi ya jezi mpya ya Taifa Stars, akisisitiza kuwa mchakato huo unapaswa kuhusisha wadau na mamlaka zinazohusika.
Kwa mujibu wa Makonda, jezi ya Taifa Stars si vazi la kawaida, bali ni sehemu ya utambulisho wa Tanzania, hivyo mchakato wa kuitengeneza, kuitambulisha na kuiuza unahitaji kupewa uzito unaostahili.
Makonda aibua maswali kuhusu mkataba
Waziri huyo amesema alijiuliza maswali 22 kuhusu mkataba unaohusiana na jezi hiyo, akisema baadhi ya changamoto zilizojitokeza zingeweza kuepukika iwapo wadau wote wangekuwa na uelewa na kushirikishwa kikamilifu katika mchakato.
Amesisitiza kuwa mjadala kuhusu jezi hiyo haupaswi kuishia katika suala la mwonekano au ubora wake pekee, bali pia unapaswa kuangalia uwezo wa kampuni au mzabuni anayesimamia mauzo yake.
Kwa mujibu wa Makonda, ni muhimu kuhakikisha jezi hiyo inawafikia Watanzania kwa urahisi kupitia mkakati madhubuti wa usambazaji na mauzo.
Akizungumzia suala la ubora wa jezi, Makonda amesema:
“Mimi ukiniambia kuhusu jezi, jezi hizi ni mbaya; cha msingi hangaikeni kutafuta jezi nzuri.”
Amesisitiza kuwa Tanzania inahitaji jezi yenye ubora pamoja na mfumo mzuri wa kibiashara utakaowezesha mashabiki kuipata kwa urahisi.
Maandalizi ya AFCON
Katika hatua nyingine, Makonda amesema maandalizi ya Tanzania kwa ajili ya michuano ya AFCON yanaendelea vizuri.
Amesema Tanzania imewekeza fedha kubwa katika kupata uenyeji wa mashindano hayo, pamoja na gharama zinazohusiana na haki za matangazo.
Kwa msingi huo, amesema masuala yote yanayohusu maandalizi ya AFCON yanaendelea kushughulikiwa na kwamba maandalizi yanaenda vizuri.