Uongozi wa Klabu ya Yanga SC umeweka wazi mipango mikubwa kuelekea msimu mpya, huku ikielezwa kuwa mfadhili wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohamed (GSM), ametenga bajeti ya takribani Sh bilioni 15 kwa ajili ya usajili wa wachezaji pekee.
Kauli hiyo imetolewa na Msemaji wa Yanga SC, Ali Kamwe, ambaye amesema Rais wa klabu hiyo, Eng. Hersi Said, aliwasiliana na GSM kuhusu mipango ya usajili wa msimu huu na kupata jibu la kupewa uhuru wa kusaka wachezaji wanaohitajika.
“Rais wetu Eng. Hersi alimuita mfadhili wetu GSM kumuuliza msimu huu tunafanyaje kusajili wachezaji. GSM akamjibu kuwa tafuta wachezaji, pesa nitatoa,” alisema Ali Kamwe.
Ali Kamwe ameongeza kuwa uwekezaji huo umeipa Yanga uwezo wa kusaka wachezaji kwa nguvu kubwa, akidai kuwa kulikuwa na mchezaji mmoja ambaye GSM alihitaji kumsajili lakini mazungumzo yalikuwa magumu kutokana na mchezaji huyo kusitasita.
“Kuna mchezaji mmoja juzi alizungumza na GSM, alimtaka ila alirukaruka, lakini tulitaka kumleta Yanga kwa jeuri ya hela aliyoweka mfadhili wetu,” alisema.
YANGA YATAMBA NA MASHAMBULIZI MAKALI
Akizungumzia kikosi cha msimu ujao, Ali Kamwe amesema mashabiki watashuhudia safu ya ushambuliaji yenye ushindani mkubwa, akitaja uwepo wa nyota kama Clement Mzize, Peter Shalulile, Mwijage, Cheikh Ibrahim Touré na Maxi Nzengeli Okello.
Amesema lengo la Yanga msimu huu ni kushinda na kwamba uwepo wa washambuliaji wengi hautakuwa tatizo kwa sababu klabu hiyo inalenga kuwa na kikosi chenye uwezo wa kushindana katika mashindano yote.
“Kuna mechi itafika tutaweka Mzize, Shalulile, Mwijage, Toure, Okello na tunashinda vizuri sana. Watu wanauliza Yanga imesajili washambuliaji watachezaje? Sisi tumedhamiria kushinda tu msimu huu,” alisema.
MZIZE NA JOB KUJIA UPYA
Kuhusu wachezaji waliokuwa majeruhi, Ali Kamwe amesema taarifa walizonazo zinaonyesha kuwa Clement Mzize na Job walitarajiwa kurejea uwanjani mwezi Desemba, lakini hali yao imekuwa nzuri kiasi cha kutoa matumaini ya kurejea mapema zaidi.
“Ripoti niliyonayo kuhusu Mzize na Job ni kuanza kucheza Desemba, lakini kwa nilivyowaona wanaweza kurudi uwanjani mapema sana kuanzia mwezi wa 10 msimu ukianza,” alisema.
YANGA DAY 2026 KUWA YA KIPEKEE
Katika hatua nyingine, Yanga imetangaza kuwa baada ya mkutano mkuu wa klabu utakaofanyika tarehe 2, itamtangaza rasmi mpinzani wa mchezo wa Siku ya Mwananchi utakaofanyika tarehe 9 katika Uwanja wa Uhuru.
Ali Kamwe amesema tamasha hilo limeongezeka thamani kutokana na usajili mkubwa uliofanywa na klabu hiyo, huku mashabiki wakipewa nafasi ya kuwaona nyota wapya wakiwa ndani ya uwanja.
Kwa upande wa tiketi, Royal Ticket inauzwa kwa Sh 300,000 ikiwa na huduma maalum kama jezi mpya ya msimu iliyosainiwa na mchezaji anayechaguliwa, usafiri wa kwenda na kurudi kutoka Serena Hotel pamoja na chakula wakati wa mapumziko.
Tiketi za VIP zinauzwa Sh 100,000 huku Mzunguko ikiwa Sh 20,000.
Yanga sasa inaendelea kujiandaa kwa msimu mpya huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuiona sura mpya ya kikosi kilichojengwa kwa uwekezaji mkubwa.