Arafat Haji Awatuliza Wananchi Kuhusu Ujenzi wa Uwanja wa Yanga Jangwani

Makamu wa Rais wa Young Africans (Yanga SC), Arafat Haji, amewatoa hofu mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuhusu maendeleo ya mradi wa ujenzi wa uwanja wa kisasa katika eneo la Jangwani, akieleza kuwa hatua muhimu za maandalizi tayari zimekamilika.

Arafat amesema Yanga na mwekezaji GSM walitia saini mkataba rasmi wa utekelezaji wa mradi huo tarehe 12, na kwa sasa maandalizi mbalimbali yanaendelea licha ya kutokuwepo kwa shughuli kubwa za ujenzi zinazoonekana eneo la mradi.

Amefafanua kuwa hali hiyo inatokana na utegemezi wa miradi mingine ya miundombinu inayotekelezwa katika Bonde la Msimbazi, ikiwemo mradi wa Mto Msimbazi na daraja jipya. Aidha, baadhi ya vifaa vitakavyotumika kujenga uwanja huo vinaandaliwa na kutengenezwa nje ya eneo la mradi kabla ya kuletwa kwa ajili ya kuunganishwa.

Kwa mujibu wa Arafat, uwanja huo utajengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ambapo sehemu kubwa ya miundombinu yake haitakuwa ya zege pekee, bali itahusisha vifaa maalumu vitakavyoagizwa kutoka nje ya nchi na kuunganishwa baada ya kukamilika kwa kazi ya kujaza eneo hadi kufikia kiwango kilichoshauriwa na wataalamu.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha uwanja unakuwa salama dhidi ya changamoto za mafuriko na athari za maji ya mvua, huku ukijengwa kwa kuzingatia viwango vyote vya kitaalamu.

Arafat amesisitiza kuwa mradi huo ni urithi mkubwa ambao uongozi wa sasa pamoja na mwekezaji GSM wanataka kuuacha kwa klabu hiyo. Amesema lengo ni kuhakikisha ndani ya miaka minne ijayo Yanga inakuwa na uwanja wake wa kisasa utakaokuwa fahari ya wanachama na mashabiki, sambamba na kuwa chanzo endelevu cha mapato kwa klabu.