Hersi Afichua Siri ya Jezi Mpya za Yanga, Asema Ubunifu Umetoka Paris

Rais wa Young Africans SC, Injinia Hersi Said, amefichua kuwa jezi rasmi za msimu mpya za klabu hiyo bado hazijaonyeshwa, akisema zile zilizowasilishwa ni maalum kwa ajili ya mazoezi ya wachezaji pekee.

Hersi amesema mashabiki wa Yanga wanapaswa kusubiri kwa hamu uzinduzi wa jezi rasmi za msimu mpya, akisisitiza kuwa zitakuwa na ubora wa hali ya juu na muonekano wa kipekee.

“Jezi mlizoziona leo ni jezi za mazoezi (Training Kit) za wachezaji wetu, si jezi rasmi za msimu mpya. Mmekwishajionea ubora wake, lakini bado makubwa yanakuja,”* alisema Hersi.

Aidha, amewapongeza wadhamini wa vifaa vya michezo GSM kwa kuhakikisha klabu hiyo inapata jezi zenye viwango vya juu, huku akieleza kuwa jezi mpya zimebuniwa na mbunifu maarufu wa mavazi kutoka Paris, Ufaransa.

“Niwapongeze sana GSM kwa kuhakikisha msimu huu tunapata jezi zenye ubora wa hali ya juu. Niwaibie siri kidogo, jezi zetu za msimu mpya zimebuniwa na mbunifu maarufu wa mavazi kutoka Paris, Ufaransa, ambaye alipewa jukumu hilo na GSM ili kuhakikisha Wananchi wanapata kitu cha kipekee,” alisema.

Hersi amesema mashabiki wa Yanga wanapaswa kusubiri uzinduzi huo kwa sababu klabu imeandaa kitu ambacho kitaendana na hadhi na historia ya timu hiyo.

*”Sasa tusubiri kwa hamu uzinduzi wa jezi rasmi za msimu mpya. Naam, mtoko unakuja na naamini utawafurahisha Wananchi wote,”* aliongeza.