Wydad Yakanusha Taarifa za Simba Kuhusu Suleiman Mwalimu

Klabu ya Wydad Athletic Club ya Morocco leo Julai 22, 2026 imetoa taarifa rasmi ikikanusha madai yaliyotolewa na Simba SC kuhusu hali ya kimkataba ya kiungo Selemani Mwalimu, ikisisitiza kuwa taarifa hiyo haiakisi ukweli wa mkataba wa mchezaji huyo.

Hatua ya Wydad imekuja baada ya Simba SC kuchapisha picha ikimuonyesha Selemani Mwalimu akisaini mkataba, ikiambatana na ujumbe uliosomeka:

“Selemani Mwalimu atakuwa sehemu ya kikosi chetu kwa msimu mwingine mmoja.”

Hata hivyo, kupitia taarifa yake rasmi, Wydad imesema haijawahi kusaini mkataba wowote wa kumtoa kwa mkopo au kwa uhamisho wa muda Selemani Mwalimu kwenda Simba SC, na kwamba hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa kati ya klabu hizo mbili kuhusu mchezaji huyo.

Aidha, Wydad imeeleza kuwa Selemani Mwalimu bado ana mkataba halali unaoendelea na klabu hiyo na ni sehemu ya mpango wa kiufundi wa kikosi cha timu ya kwanza.

“Timu ya ufundi inaendelea kufanya kazi ya kumrejesha mchezaji huyo kwenye kikosi kulingana na programu iliyowekwa na uongozi wa klabu,” sehemu ya taarifa hiyo imeeleza.

Wydad pia imesisitiza kuwa itachukua hatua zote zinazostahili kulinda maslahi yake kwa mujibu wa sheria, huku ikiwataka mashabiki na vyombo vya habari kutegemea taarifa rasmi zinazotolewa na klabu hiyo na kuepuka kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa.

Mvutano huo unaibua sintofahamu kuhusu hatma ya Selemani Mwalimu, baada ya Simba kutangaza hadharani kuwa ataendelea kuwa sehemu ya kikosi chake kwa msimu ujao, huku Wydad ikisisitiza kuwa mchezaji huyo bado yupo chini ya mkataba wake na hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili.