Lewis Hamilton Avunja Ukimya Baada ya Ushindi Wake wa Kwanza Ferrari

Nyota wa Formula One, Lewis Hamilton, ameonyesha hisia zake baada ya kupata ushindi wake wa kwanza akiwa na timu ya Ferrari, akieleza kuwa ni moja ya nyakati za kipekee zaidi katika maisha yake ya mbio.

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Hamilton alisema amekuwa akiota kufanikisha jambo ambalo wengi waliliona haliwezekani, huku akiwashukuru viongozi, wahandisi na wafanyakazi wote wa Ferrari kwa juhudi zao kubwa zilizomfikisha kwenye mafanikio hayo.

“Siwezi hata kueleza jinsi ninavyojisikia baada ya hatimaye kushinda nikiwa nimevaa rangi nyekundu. Asanteni sana Ferrari kwa kazi kubwa mliyoifanya hapa Barcelona na Maranello. Ari na kujitolea kwenu vinaanza kuzaa matunda, na huu ni mwanzo tu,” alisema Hamilton.

Bingwa huyo wa dunia mara kadhaa pia aliwapa shukrani mashabiki wake waliompa nguvu katika nyakati ngumu za maisha na taaluma yake, akisisitiza kuwa ushindi huo si wake peke yake bali ni wa kila aliyesimama naye katika kipindi chote cha changamoto.

Hamilton alikiri kuwa kulikuwa na nyakati ambazo alihisi kukata tamaa kutokana na ukosoaji na presha mbalimbali, lakini mashabiki wake waliendelea kumtia moyo kupambana na kutokata tamaa.

“Kulikuwa na nyakati za giza, nyakati ambazo nilihisi sina thamani na matumaini yalionekana kutowezekana. Lakini nyinyi mlinikumbusha kuendelea kupigana na kutokukata tamaa. Ushindi huu ni wenu kama ulivyo wangu,” aliongeza.

Mwisho, Hamilton aliwashukuru mashabiki wa Ferrari maarufu kama Tifosi pamoja na kundi lake la mashabiki wa Team LH kwa kuendelea kumuunga mkono, huku akiahidi kuwa ushindi huo ni mwanzo wa mafanikio mengine makubwa yajayo.