Aliyekuwa nyota wa zamani wa Leicester City na Wolverhampton Wanderers, Ben Marshall, ameepuka kifungo cha jela baada ya kuvamia duka la vitu vya kale na kuliharibu vibaya akiwa katika hali ya ulevi.
Tukio hilo lilitokea Februari 4 mwaka huu mjini Newport, Shropshire, ambapo Marshall mwenye umri wa miaka 35 alivamia duka la antiques lijulikanalo kama Junk & Disorderly na kusababisha uharibifu wenye thamani ya zaidi ya pauni 7,000.
Mahakama ilielezwa kuwa mchezaji huyo wa zamani, aliyewahi pia kuichezea Stoke City, alikuwa ametumia usiku wake kunywa pombe kabla ya kufanya tukio hilo lililoelezwa kuwa “shambulio baya”.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Marshall alivunja mlango wa kioo wa mbele kwa mateke kabla ya kuingia ndani ya duka hilo na kuanza kuharibu mali mbalimbali ikiwemo kamera za CCTV, mashine ya zamani ya kuhifadhia fedha pamoja na bidhaa zilizokuwa kwenye rafu.

Hasara hiyo iliongezeka zaidi baada ya duka kufungwa kwa siku mbili kutokana na uharibifu huo.
Licha ya kukiri makosa ya kuvamia eneo kwa nia ya kuharibu mali pamoja na uharibifu wa mali, mahakama ya Telford Magistrates’ Court ilimpa adhabu ya kifungo cha nje kwa miezi 12 badala ya jela.
Marshall ameagizwa kuhudhuria programu ya matibabu ya matumizi ya pombe kwa miezi sita, kufanya saa 120 za kazi za kijamii bila malipo pamoja na kulipa fidia ya pauni 1,500.
Akitoa hukumu hiyo, mwenyekiti wa baraza la mahakama, Steven Jonas, alisema tukio hilo lilikuwa la kusikitisha na kwamba Marshall “alipoteza kabisa udhibiti na kusababisha uharibifu mkubwa.”
