Algeria Yaizima Jordan na Kufufua Matumaini ya Kufuzu Kombe la Dunia 2026

TIMU ya taifa ya Algeria imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Jordan katika mchezo wa Kundi J uliopigwa kwenye Uwanja wa Levi’s Stadium, Santa Clara.

Katika pambano hilo la timu mbili za Kiarabu, Jordan walikuwa wa kwanza kupata bao kabla ya mapumziko lakini walishindwa kulinda uongozi wao kipindi cha pili, huku Algeria ikitumia udhaifu wa wapinzani wao katika mipira ya adhabu kugeuza matokeo.

Mchezo ulianza kwa kasi huku timu zote zikihitaji ushindi ili kuendelea kuwa na matumaini ya kusonga mbele. Jordan walitengeneza nafasi mapema kupitia kichwa cha Nizar Al-Rashdan kilichopita karibu na lango la kipa Luca Zidane, wakati Algeria walijibu haraka kupitia Amine Gouiri ambaye alipiga shuti lililoishia pembeni mwa nyavu.

Jordan walicheza kwa mfumo wao wa kawaida wa 5-4-1, wakijikita zaidi kwenye ulinzi na mashambulizi ya kushtukiza wakimtegemea nyota wao Mousa Al-Tamari.

Dakika ya 40 Jordan walifanikiwa kuvunja ukimya baada ya kosa la Ramiz Zerrouki kupokonywa mpira na Mohannad Abu Taha. Al-Tamari alihusika katika shambulizi hilo kabla ya mpira kumkuta Al-Rashdan ambaye alimalizia kwa ustadi na kuandika bao la kwanza.

Kipindi cha pili Algeria walitawala mchezo kwa umiliki mkubwa wa mpira lakini walikumbana na ukuta mgumu wa safu ya ulinzi ya Jordan.

Hata hivyo, dakika ya 69 Algeria walisawazisha kupitia Nadji Benbouali aliyefunga kwa kichwa baada ya kupokea krosi safi ya Riyad Mahrez kutoka katika mpira wa adhabu.

Shinikizo la Algeria liliendelea na dakika ya 82 walipata bao la ushindi kupitia Amine Gouiri. Krosi ya Anis Hadj Moussa ilimpata Ramy Bensebaini ambaye alipiga kichwa kilichomkuta Gouiri na kufunga akiwa karibu na lango.

Wachezaji wa Jordan walipinga wakidai Gouiri alikuwa ameotea, lakini baada ya uchunguzi wa VAR bao hilo lilithibitishwa kuwa halikuwa la kuotea.

Jordan walijaribu kutafuta bao la kusawazisha katika dakika za mwisho lakini walishindwa kuvunja safu ya ulinzi ya Algeria.

Ushindi huo unaifanya Algeria kuingia katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya Austria ikiwa na matumaini makubwa ya kufuzu hatua inayofuata.

Kwa upande wa Jordan, matokeo hayo yanamaanisha wameondolewa rasmi kwenye mbio za kufuzu hatua ya 32 bora licha ya kuwa bado wana mchezo mmoja uliobaki dhidi ya Argentina.