KOCHA SIMBA AANZA NA MAJEMBE HAYA YA KAZI

KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco,ameweka wazi kuwa atakuwa na programu maalum na majembe mapya ya kikosi hicho ili kuhakikisha wanaingia katika mfumo wake na kupata muunganiko wa pamoja wa timu ili kuwa na kikosi imara.


Simba, Jumatano
ilianza vizuri vita ya kuwania ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Selem View Academy, ambapo leo Ijumaa Simba wanatarajia kuvaana na Mlandege majira ya saa 2:15 usiku huku ikihitaji kushinda mchezo huu ili kukata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo.


Katika mchezo huo 
wa juzi, Simba ilijaribu baadhi ya mastaa wapya ambao wapo kwenye majaribio ambao ni; Sharraf Shiboub na Muivory Coast, Mounkoro Tenena, ambao kuna uwezekano wakasajiliwa katika kipindi cha dirisha hili dogo la usajili.

Kocha Pablo alisema: “Tupo kwenye kipindi cha usajili wa dirisha dogo, ni wazi kuwa matumaini ya kocha yoyote ni kuhakikisha anakuwa na kikosi bora, ndicho ambacho tunakifanya kwa sasa kwa kujaribu kuona ni nyota gani tunawasajili kwa ajili ya kuboresha kikosi chetu.


“Baada ya kukamilisha 
mchakato wa kusajili wachezaji bora, kazi kubwa itakayobaki kwangu kama kocha ni kuhakikisha natengeneza muunganiko, ambapo tayari nimeandaa programu maalum ili kupata matokeo bora kutoka kwa kila mchezaji.”