>

MAYELE NA KAGERE WAPO KWENYE VITA YAO

WASHAMBULIAJI wawili ndani ya timu zenye maskani yake pale Kariakoo Yanga na Simba wapo kwenye vita nzito ya kutafuta ufalme wa kutupia mabao kutokana na kasi yao ya kutupia kwa Fiston Mayele wa Yanga na Meddie Kagere wa Simba kuzidi kuwa kubwa.

Mfalme kwenye suala la kutupia kwa msimu uliopita ni nahodha wa Simba, John Bocco ambaye ni mzawa na alitupia mabao 16 na pasi mbili za mabao msimu wa 2020/21.

Mayele raia wa DR Congo amecheza mechi 10 akitumia dakika 737 na ametupia mabao manne na pasi moja ya bao na kuhusika kwenye mabao matano kati ya 16 ambayo yamefungwa na timu hiyo.

Mabao hayo manne mawili amefunga nje ya 18 na mawili amefunga akiwa ndani ya 18 na hata pasi yake moja alitoa akiwa nje ya 18 ilikuwa Uwanja wa Majimaji, Songea mbele ya KMC.

Kwa upande wa Kagere raia wa Rwanda amecheza mechi 9 akitumia dakika 486 mabao manne na pasi moja ya bao ambayo aliitoa mbele ya Ruvu Shooting na mtupiaji alikuwa ni Kibu Dennis.

Kagere ana zali akiwa ndani ya 18 kwa kuwa mabao yake yote pamoja na pasi ametoa akiwa kwenye eneo hilo na kumfanya ahusike kwenye mabao matano kati ya 12 ambayo yamefungwa na timu ya Simba.