UNGANISHA MIGUU NA KICHWA CHA AJIBU ILI TUPATE MAJIBU

IBRAHIM Ajibu Migomba, sasa ametua Azam FC kwa mkataba wa mwaka mmoja akiandika rekodi ambayo wameiweka wachezaji
wachache sana iwe kwa wazalendo au wa
kigeni.

Tayari sasa ameandika rekodi ya kuzichezea timu zote tatu kubwa za Dar es Salaam au Tanzania, nazungumzia Simba, Yanga na sasa Azam FC.

Simba amekulia, amecheza au kukaa muda mrefu zaidi. Aliondoka kwenda Yanga ambako alifikia hadi kuwa nahodha kabla ya kuamua
kurejea tena ‘nyumbani’ Msimbazi.

Sasa kamalizana na matajiri wa Chamazi, yaani Azam
FC. Kwa timu hizi tatu na kama umewahi kucheza
timu ya taifa, unaweza kusema umemaliza kila kitu labda uzungumzie kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania au Afrika.

Tuangalie wakati Ajibu anaandika rekodi hiyo, ana rekodi nyingi ya aina yake ambayo huenda itabaki kwake au atabaki nayo mwenyewe tu. Kwamba ni mchezaji ambaye hajawahi
kulaumiwa kuhusiana na kuujua mpira.

Kila mmoja ukimuuliza, atakuambia Ajibu anaujua
mpira, lakini mara zote yuko benchi. Mara kadhaa ambazo amekuwa akipata nafasi ya kucheza, anaweza kufanya vizuri kwa siku chache, baada ya hapo utasikia, hafanyi vizuri
tena na mwisho itakuwa anaonekana benchi
mara nyingi ikiwezekana hata jukwaani kabisa.

Mara nyingi, kwa wale kama mimi ambao tumekuwa tukisema ukweli, tunaonekana tunamsakama lakini ukweli unaweza kuwa
dawa kuliko unafiki uliojaa tabasamu.

Sote tunakiri ana uwezo, hata waliomchukua Azam FC wanaamini kama wewe na mimi lakini bahati mbaya inaonekana, wanaomzunguka Ajibu wameshindwa kumsaidia kwa kuwa muda
mwingi wanajaribu kumuonyesha anaonewa badala ya kumuelezea anapokosea.

Hana mwendelezo wa ubora, hilo halina ubishi na mifano yake ipo hadharani. Kwamba akianza kuonyesha kiwango bora, baada ya kusifiwa au kuwa gumzo anaporomoka. Hii imejionyesha
alikuwa Simba kwa kuwa ni muda mrefu, alipokuwa Yanga na hata baada ya kurudi Simba.

Makocha wamepita wengi tofauti, hawakuwa
wakiona kuna sababu ya kumuacha. Kama ni
tuzo ya uvumilivu huenda walipaswa kupewa
Simba kutokana na kumvumilia na ikiwezekana
kumsajili tena na tena licha ya kwamba faida
yake kwao ilionekana ni ndogo. Huenda
walikuwa na subira wakiamini ataamka hadi
kuwa tegemeo kabisa kwao, naona
imeshindikana.

Karata ya mwisho ya Ajibu ni Azam FC, hii
inaweza kuwalazimisha Simba kumrudisha kwa
dau kubwa au Yanga wakamkumbuka tena
nahodha wa zamani au naye akafungua moyo
na kutazama nje ya Tanzania. Lakini kama
atashindwa kuunganisha moyo na miguu yake,
lazima jibu halitakuwa zuri kwake na masikioni
mwetu.

Yes, aunganishe. Maana kama miguu yake
itaamua inavyotaka, moyo wake ukawa na
mawazo tofauti na yanayotakiwa na miguu
yake, kutakuwa na mgongano ambao mwisho
utabakiza ile hadithi ya “Ajibu anajua sana
mpira lakini sijui kwa nini!”

Wamekuja wengi wakapita Simba au Yanga na
kwenda kuuzwa kwa mamilioni au mabilioni ya
fedha nje Tanzania. Sasa sisi kwa nini
ishindikane kwa mzalendo Ajibu ambaye kabisa
tunaona kiwango chake ni bora ikiwezekana
wakati mwingine kuliko wao?

Mnaomzunguka Ajibu mwelezeni ukweli,
msimpende kwa kumdanganya na matabasamu
ya kinafiki. Mwambieni Azam FC ni karata ya
mwisho la sivyo itakuwa ndio mwisho wake wa
kusimama juu na safari ya kurejea chini itaanza.

Ninaamini Ajibu anajitambua na anajua amekosea wapi, haiwezekani awe benchi Simba, Yanga halafu Simba tena halafu akakae benchi na Azam FC. Anatakiwa abadilike na
kufanya kazi inayomuaminisha. Binafsi nimeona hata Azam FC bado hawamuamini maana wamempa mkataba wa mwaka mmoja tu wakati umri unamruhusu hata zaidi ya miaka
mitatu!