>

UBORA WA SIMBA WATAJWA KUWA UPO KWENYE VIUNGO

ABDALAH Mohamed, ‘Bares’ Kocha Mkuu wa JKT Tanzania amesema kuwa ubora wa Simba upo kwenye viungo jambo ambalo liliwafanya washindwe kupata matokeo mazuri walipokutana nao Uwanja wa Mkapa.

Simba Desemba 14 iliweza kushinda bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho raundi ya tatu ambapo bao la ushindi lilifungwa na Kibu Dennis.

Kwenye mchezo huo viungo ambao waliweza kuonyesha uwezo wao ni pamoja na Sadio Kanoute,Peter Banda,Mzamiru Yassin,Pape Sakho.

Akizungumza na Saleh Jembe, Bares amesema kuwa uimara wa Simba upo kwenye eneo la viungo jambo ambalo aliligundua mapema na kuwazuia wasiweze kuwapa tabu kwenye mchezo wao.

“Nilitambua kwamba ubora wa Simba upo kwenye viungo hivyo jambo ambalo nilifanya ni kuweza kuwazuia kwa nidhamu ili tusiweze kufungwa lakini makosa ambayo tulifanya ni kushindwa kutumia nafasi ambazo tulizipata.

“Tulistahili kushinda lakini kwa kuwa wapinzani wetu wameshinda wanastahili pongezi.Baada ya kupoteza mchezo wetu hesabu zetu ni kwenye mechi zijazo hivyo tunaamini kwamba tutafanya vizuri,” amesema Bares.

Simba ni mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho ambapo walilitwaa baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya watani zao wa jadi Yanga kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, mwisho wa reli Kigoma.