SALAH AGOMA KUSEPA LIVERPOOL

STAA wa Liverpool raia wa Misri, Mohamed Salah ameweka wazi kuwa kwa sasa hafikirii kuondoka ndani ya Liverpool na badala yake anahitaji kumaliza soka akiwa ndani ya timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Jurgen Klopp.

Salah amebainisha kuwa ikitokea siku akasepa ndani ya timu hiyo kisha siku akacheza na timu ambayo amehamia kwa wakati huo dhidi ya Liverpool ambao walikuwa ni mabosi zake atajisikia vibaya jambo ambalo hapendi kuona likitokea kwenye maisha yake.

Mkataba wake ndani ya kikosi cha Liverpool unatarajiwa kumeguka mwaka 2023 inatajwa kuwa mabosi wa timu hiyo wanahitaji kumuongezea mkataba mwingine ili aweze kuendelea kukiwasha ndani ya timu hiyo.

Salah alikuwa anatajwa kuibukia Real Madrid ama Barcelona ikiwa dili lake lingeweza kujibu ila kwa maneno ambayo ameyasema ni uhakika kwamba ataongeza mkataba mpya nyota huyo ambaye amedumu ndani ya Liverpool kwa muda wa misimu mitano mpaka sasa akiwa ametupia mabao zaidi ya 100.

“Kama ukiniuliza kuhusu Liverpool basi nitakwambia kwamba napenda kuwa hapa mpaka siku yangu ya mwisho ya kucheza soka. Lakini siwezi kusema zaidi kwa sababu hilo lipo nje ya uwezo wangu,”.

Liverpool leo ina kibarua cha kusaka ushindi mbele ya Manchester United kwenye mchezo wa Ligi Kuu England unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Old Trafford saa 12:30 jioni huku nyota huyo akipewa nafasi kubwa ya kuweza kuanza kikosi cha kwanza.