UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa unahitaji ushindi mbele ya Red Arrows ili uweze kufikia malengo ya kutinga hatua ya makundi katika Kombe la Shirikisho.
Leo Desemba 5 Simba ina kazi ya kusaka ushindi mbele ya Red Arrows kwenye mchezo wa marudio unaotarajiwa kuchezwa nchini Zambia wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Mabao hayo yalifungwa na Bernard Morrison ambaye alifunga mawili na moja ni mali ya Meddie Kagere.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amesema kuwa wanaamini kwamba watashinda mchezo wao dhidi ya Red Arrows ambao utakuwa ni tiketi kwao kutinga hatua ya makundi.
“Tunaamini kwamba tutapata matokeo mbele ya Red Arrows licha ya kwamba tutakuwa ugenini, kikubwa ambacho tunaomba ni dua kwa Watanzania na kila mmoja kuwa bega kwa bega nasi ili tuweze kupata ushindi.
“Hakuna mabadiliko kwenye kikosi zaidi ni mwalimu mpya ambaye yupo, sasa ikiwa kunakuwa na kocha mpya lazima kuwe na tofauti, wachezaji wanaonekana kwa sasa wanapambana na saikolojia zao zipo sawa kwa ajili ya mechi za ushindani kikubwa kwa mashabiki dua muhimu,” amesema Barbra.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa leo Uwanja wa Heroes ambapo kinachohitajika ni Simba kushinda ushindi wa namna yoyote ile ama sare ya aina yoyote ile.