MAKAMBO APIGA HESABU HIZI KUELEKEA DESEMBA 11

 

HERITIER Makambo, mshambuliaji wa Yanga ameweka wazi kuwa ikiwa atapata nafasi ya kuanza kwenye mchezo wa Kariakoo, Dabi Desemba 11 mbele ya Simba atapambana kwa kushirikiana na wachezaji wenzake ili kupata ushindi.

Hesabu hizo ndefu za Makambo zinakuja ikiwa zimebaki siku tano kabla ya mchezo huo kuchezwa Uwanja wa Mkapa ambapo Yanga imekuwa kwenye kasi ya kupata ushindi kwenye mechi sita na kulazimisha sare moja na ipo nafasi ya kwanza na pointi zake kibindoni ni 19.

Makambo amesema kuwa wanahitaji kufanya vizuri kwenye mechi zote ambazo watacheza ndani ya ligi ikiwa ni pamoja na mchezo wao ujao dhidi ya Simba.

“Nimejipanga vizuri sana na sio mimi peke yangu bali ni timu nzima tumejiandaa kwaajili ya kuhakikisha timu inapata alama tatu za mchezo huo, (Simba) kwa sababu pointi hizo tatu zina umuhimu mkubwa kwetu katika kuhakikisha tunafikia malengo yetu ya kutwaa ubingwa.

“Hivyo mimi binafsi kama nikipata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha Nabi, (Nasreddine) nitahakikisha ninapambana ili niweze kuipatia timu yangu ushindi kwa hali na mali.

“Kuhusu ligi kweli ni ngumu lakini nina imani kwa maandalizi yetu tuliyonayo na tunaendelea kujipanga vizuri jambo linalotupa imani kwamba tutashinda, unajua hii mechi itakuwa ngumu sana lakini hatuna budi kupambana ili kuendana na matakwa ya timu,” amesema Makambo.

Nyota huyo bado hajapata bahati ya kufunga bao ndani ya ligi kati ya yale 12 ambayo yamefungwa kwa msimu wa 2021/22.