MTIBWA SUGAR WANAHITAJI MAOMBI

UONGOZI wa Mtibwa Sugar umeweka wazi kuwa kwa sasa unahitaji maombi ya Watanzania ili waweze kurejea kwenye ubora wakiwa uwanjani.

Kwenye msimamo Mtibwa Sugar ikiwa imecheza jumla ya mechi saba imekusanya pointi mbili pekee jambo ambalo linawapa tabu mashabiki na mabosi wa timu hiyo.

Haijaambulia ladha ya ushindi mpaka wakati huu ambapo ipo nafasi ya 16 ikiwa inafunga dimba kwenye timu zote ndani ya ligi kwa msimu wa 2021/22.

Thobias Kifaru, Ofisa Habari mkongwe na mjuzi katika fani hiyo ameweka wazi kwamba kwa mwendo ambao wanakwenda nao Mtibwa Sugar haufurahishi hivyo wanahitaji maombi.

“Kiukweli timu yetu ipo vizuri hasa kwa upande wa wachezaji lakini kwa matokeo ambayo tunayapata tunahitaji maombi ili kuweza kurejea kwenye ubora wetu.

“Wachezaji wanauwezo mkubwa na wanajua kufanya kazi kwa kujituma lakini bahati bado haijawa upande wetu, imani yetu ni kwamba kwa wakati ujao kila kitu kitakuwa sawa,” amesema.

Mchezo wao uliopita Mtibwa Sugar ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.

Ina wachezaji wenye uwezo ikiwa ni pamoja na Said Ndemla pamoja Ibrahim Ame ambaye ni beki wa kati wakiwa pamoja na Salum Kihimbwa, Baraka Majogoro.