Mataifa Yaliyoingiza Timu Mbili Katika Hatua Ya Pili Ya Mtoano Ligi ya Mabingwa

Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika CAF Champions League imefikia hatua ya kusisimua baada ya kukamilika kwa raundi ya kwanza ya mchujo.

Mataifa makubwa ya soka yameonyesha ubabe kwa kufanikiwa kuingiza klabu zake zote mbili katika raundi ya pili ya mtoano ili kuwania nafasi ya kuigia makundi

Tanzania imewakilishwa vyema na klabu zake kongwe za Young Africans SC na Simba SC. Young Africans SC ilitinga hatua hii baada ya kuiondoa Gaborone United kwa jumla ya mabao 3-2, huku Simba SC ikionyesha kiwango cha juu kwa kuisambaratisha Mighty Wanderers kwa jumla ya mabao 7-1.

Afrika Kusini imeingiza timu zake mbili zenye upinzani mkubwa barani Afrika ambazo ni Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates. Mamelodi Sundowns ilifuzu moja kwa moja hadi hatua hii bila kucheza raundi ya awali, wakati Orlando Pirates ilipita kwa kishindo baada ya kuzifumania nyavu na kuwatoa La Cure Sylvester.

Misri inaendeleza utawala wake katika soka la Afrika kupitia klabu za Zamalek SC na Pyramids FC. Zamalek SC ilisonga mbele kwa kuifunga AS du Port ya Djibouti, huku Pyramids FC ikionyesha ukali wake kwa kuifunga Gor Mahia kwa jumla ya mabao 7-1.

Mechi za mkondo wa kwanza wa hatua hii ya pili ya mtoano zitachezwa kati ya Oktoba 16–18, 2026, na mechi za marudiano zitapigwa kati ya Oktoba 23–25, 2026. Washindi wa jumla watakata tiketi ya kucheza hatua ya makundi.