Mchezaji wa Yanga, Mohamed Hussein, amesema timu hiyo inaendelea vizuri na ipo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Geita Gold, licha ya kuwa na muda mfupi wa maandalizi.
Mohamed amesema maandalizi yaliyofanyika katika siku mbili zilizopita yamewasaidia kujiandaa vyema kwa mchezo huo na kuongeza kuwa benchi la ufundi limefanya uchambuzi wa kina kuhusu wapinzani wao.
“Ni kweli hatukuwa na muda mrefu wa kufanya maandalizi makubwa, lakini tunaamini maandalizi ya jana na leo yatatusaidia kuwa tayari kwa mchezo wa kesho,” amesema Mohamed Hussein.

Akizungumzia Geita Gold, Mohamed amesema ni timu yenye ubora na wachezaji wenye uwezo mkubwa, hivyo Yanga haiwezi kuichukulia mchezo huo kwa wepesi.
“Geita Gold ni timu nzuri. Tumefuatilia baadhi ya michezo yao na tumeona wana wachezaji wazuri ambao mmoja mmoja wanafanya vizuri, lakini kwa ujumla pia ni timu yenye ubora.
“Tumemchambua mpinzani wetu kwa ukaribu. Tumebaini baadhi ya nguvu na mapungufu yao, hivyo tunakwenda kuyafanyia kazi ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri katika mchezo wa kesho,” ameongeza.