Kocha Mngqithi Aibuka Na Mbinu Mpya Yanga, Awataka Mashabiki Kuwa Na Subira

Kocha Mkuu wa Young Africans SC, Manqoba Mngqithi, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kufuatia kiwango kisichoridhisha katika baadhi ya michezo, akisema amepata “akili mpya” ya kukisuka na kukiunganisha vizuri kikosi chake ili kucheza soka la kuvutia na kupata matokeo makubwa zaidi.

Mngqithi, raia wa Afrika Kusini, amekiri kuwa timu yake bado inakabiliwa na changamoto ya kutengeneza na kutumia nafasi za kufunga mabao, huku safu ya ushambuliaji ikishindwa kutumia ipasavyo baadhi ya nafasi zinazopatikana.

Hali hiyo imezua malalamiko miongoni mwa mashabiki, hasa kutokana na mabadiliko ya wachezaji yanayofanywa na benchi la ufundi katika michezo ya hivi karibuni.

Yanga imefanikiwa kutinga hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuiondoa Gaborone United ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-2. Yanga ilitoka sare ya 1-1 katika mchezo wa ugenini kabla ya kushinda 2-1 nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Licha ya kufuzu, kiwango cha soka kilichoonyeshwa na Yanga hakikuwafurahisha mashabiki wengi, ambao walionyesha kutoridhishwa na baadhi ya maamuzi ya benchi la ufundi, hususan mabadiliko ya wachezaji.

Akizungumzia hali hiyo, Mngqithi amesema kikosi chake bado hakijafikia kiwango cha utayari wa asilimia 100, lakini anaamini mbinu mpya alizozipata zitasaidia kuwaunganisha vizuri wachezaji na kuongeza makali katika eneo la umaliziaji.

Kocha huyo amewataka mashabiki wa Yanga kuwa na subira na kuendelea kuiunga mkono timu, akisisitiza kuwa kikosi kinaendelea kujengwa na kuimarika kadiri msimu unavyoendelea.