Job na Mzize Kuongeza Nguvu Yanga Baada ya Kufanyiwa Vipimo Afrika Kusini

.Beki wa kati ndani ya kikosi cha Yanga SC, Dickson Job na mshambuliaji Clement Mzize wanatarajiwa kurejea uwanjani hivi karibuni baada ya kufanyiwa vipimo nchini Afrika Kusini.

Wachezaji hao wa Yanga SC walikosekana kwenye mechi 5 za ligi 2026/27 kutokana na kutokuwa fiti tayari walianza mazoezi chini ya uangalizi wajopo la madaktari la Yanga SC. Nyota hao walikosekana kwenye mchezo dhidi ya Gaborone United walipotoshana nguvu kwa kufungana 1-1 Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ali Kamwe, Menej awa Idara ya Habari na Mawasiliano Yanga SC amesema wachezaji hao tayari wamefanyiwa vipimo wanajiandaa kurejea uwanjani kuendelea na majukumu ya kazi.

“Kuna habari njema kutoka kwa wataalamu wetu wa masuala ya kitabibu wanasema kuwa wachezaji wetu Dickson Job na Clement Mzize, ambao walisafiri kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya vipimo, wapo salama na wanajiandaa kurejea uwanjani.

“Kimsingi, wachezaji hawa wawili ni kama usajili mpya kwetu, wale ambao mmecheza na Yanga na hamkukutana na Clement Mzize Bull Striker basi niwaambie tu kwamba Mzize na Job wamerudi,” alisema Kamwe.

Yanga SC kwenye msimamo wa ligi inaongoza ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi 5 imeshinda zote msimu wa 2026/27. Mchezo wa kwanza ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo FC.

Mchezo ujao kwa Yanga SC ni dhidi ya Gaborone United ya Botswana mechi ya  mkondo wa pili Ligi ya Mabingwa Afrika unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex, Septemba 12, 2026 saa 1:00 usiku umepewa jina la Sele Day mfungaji wa bao pekee dhidi ya Gaborone, ugenini.

Stori na Lunyamadizo Mlyuka