Baraza la Michezo Laibua Jingine Simba! “Serikali Imekamilisha Wajibu Wake” – Video

Dar es Salaam: Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limetoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa Katiba ya Klabu ya Simba iliyofanyiwa marekebisho na kuidhinishwa rasmi Februari 18, 2026.

Kwa mujibu wa BMT, marekebisho hayo yalipitishwa na Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Simba uliofanyika Novemba 30, 2025, kabla ya kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama na Vilabu vya Michezo kwa ajili ya uchambuzi na hatua zaidi za kisheria.

BMT kupitia Msajili ilikamilisha mchakato wa uchambuzi wa kisheria, kuidhinisha na kukabidhi rasmi Katiba hiyo kwa Klabu ya Simba Februari 18, 2026.

Baraza hilo limeeleza kuwa baada ya kukamilisha jukumu lake la kisheria, sasa utekelezaji wa Katiba hiyo pamoja na kukamilisha mabadiliko yaliyopitishwa ni jukumu la wanachama na Klabu ya Simba yenyewe.

BMT imefafanua kuwa iko tayari kutoa maelekezo na ufafanuzi wa taratibu pale utakapohitajika, lakini imeitaka Simba kutumia vyombo na taratibu zake halali katika kukamilisha utekelezaji wa Katiba hiyo.

Aidha, Serikali kupitia BMT imeahidi kuendelea kusimamia maendeleo ya michezo nchini kwa kuzingatia sheria, uwazi, uwajibikaji na maslahi ya wananchi.

Hatua hiyo ya BMT imekuja wakati ambapo utekelezaji wa marekebisho ya Katiba ya Simba ukiendelea kuwa suala muhimu ndani ya klabu hiyo, huku wanachama wakitarajiwa kutumia taratibu zilizowekwa kikatiba katika kukamilisha mchakato huo.