Harry Kane Kufanya Mazungumzo ya Kuongeza Mkataba Bayern Munich

 

Mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane, amesema yuko tayari kuanza mazungumzo na mabingwa hao wa Bundesliga kuhusu kuongeza mkataba wake.

Kane mwenye umri wa miaka 33 amebakiza miezi 12 kwenye mkataba wake wa miaka minne aliosaini baada ya kuhamia Bayern Munich akitokea Tottenham Hotspur kwa ada ya pauni milioni 86.4 mwezi Agosti 2023.

Msimu uliopita, Kane alikuwa katika kiwango bora, akifunga mabao 61 katika mechi 51 katika mashindano yote, huku Bayern Munich ikifanikiwa kushinda mataji ya Bundesliga na Kombe la Ujerumani.

Kane amesema pande zote mbili zilikubaliana kuanza mazungumzo baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia na likizo yake, hivyo anatarajia mchakato huo kuanza ndani ya wiki hii au ijayo.

“Tulisema tunataka kuzungumza baada ya Kombe la Dunia na baada ya likizo yangu. Kwa hiyo sina uhakika ni lini hasa, lakini wataanza wiki hii au ijayo. Tutaianza mazungumzo,” Kane alisema.

Mshambuliaji huyo amesema hana wasiwasi kuhusu mustakabali wake, akieleza kuwa yeye pamoja na Bayern Munich wako katika hali ya utulivu kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, Kane amekiri kuwa muda wa kuanza mazungumzo umefika kutokana na kubakiwa na mwaka mmoja pekee katika mkataba wake.

“Pande zote mbili ziko tulivu na nina uhakika kutakuwa na mazungumzo wiki hii au ijayo,” alisema Kane.

Hatua hiyo inafungua uwezekano wa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England kuendelea kubaki Allianz Arena, ambako ameendelea kuwa mhimili muhimu wa safu ya ushambuliaji ya Bayern Munich tangu alipojiunga na klabu hiyo.