Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, akieleza kuwa ana imani na uwezo wa wachezaji wake katika kukabiliana na presha ya Kariakoo Derby.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 11, mjini Zanzibar, Mngqithi amesema maandalizi ya timu yake yamekwenda vizuri licha ya kuwa na muda mfupi wa kujiandaa kutokana na ratiba ya mechi za mwishoni mwa wiki.
Amesema hali hiyo si kwa Yanga pekee, bali hata Simba imekuwa na muda mfupi wa maandalizi, hivyo anaamini mchezo huo utakuwa wa kuvutia kutokana na mazingira ambayo timu zote zimekutana nayo.
“Tunajiamini kwa sababu tuna timu nzuri, tuna wachezaji wenye uzoefu na wanaoweza kuhimili presha yoyote katika mchezo wa kesho,” amesema Mngqithi.
Kocha huyo amesema huu utakuwa mchezo wake wa kwanza wa Kariakoo Derby tangu alipokabidhiwa jukumu la kuiongoza Yanga, jambo analoliona kuwa fursa ya kuanza ukurasa mpya katika moja ya mechi kubwa za soka nchini.
“Habari za asubuhi kwa wote. Hii ni mara yangu ya kwanza kushiriki katika Derby hii, hivyo nina hamu kubwa ya kuona kitakachotokea,” amesema.
Mngqithi amesema pamoja na muda mfupi wa maandalizi, anaamini Yanga ina kikosi chenye uwezo wa kucheza soka zuri na la kuvutia.
“Tuna imani kubwa na timu yetu. Tuna kikosi chenye uwezo wa kucheza soka zuri na la kuvutia,” amesema.
Amesema pia anatamani kuona timu yake ikicheza soka litakalowavutia mashabiki na kuwapa sababu ya kujitokeza uwanjani.
“Zaidi ya kutaka kushinda mechi, mimi ni kocha ninayependa sana soka zuri. Nataka kucheza aina ya soka ambayo itawafanya watu wawe na sababu ya kuacha shughuli zao, kutoka majumbani kwao na kuja uwanjani kutazama timu yao ikicheza,” amesema Mngqithi.
Kuhusu Simba, Mngqithi amesema anatambua ubora na mwenendo mzuri wa wapinzani wao, lakini ameona baadhi ya tofauti katika namna wanavyocheza.
“Ni kweli wapinzani wetu wamekuwa na mwenendo mzuri, lakini naamini kuna baadhi ya tofauti kubwa ambazo nimeziona katika namna wanavyocheza. Lakini kwa ujumla tunawaheshimu na tunatambua ubora wao,” amesema.
Ameongeza kuwa Yanga haijaenda Zanzibar kwa ajili ya kushiriki tu, bali kwa lengo la kushindana na kuhakikisha inafanya vizuri katika mchezo huo.
“Naweza kuwaahidi mashabiki wetu kwamba hatukuja hapa kwa ajili ya kushiriki, tumekuja hapa kushindana na kuwapa Simba changamoto kubwa na lengo letu ni kuhakikisha tunafanya vizuri na kulitetea taji hili,” amesema.
Mchezo huo wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Simba utachezwa kesho, Agosti 12, katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kuanzia saa 2:30 usiku.
Aidha, Yanga imewataka mashabiki wake kujitokeza kwa wingi uwanjani na kuisapoti timu katika dakika zote za mchezo.
“Tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani kesho, watusapoti na kuwa nyuma yetu katika kila dakika ya mchezo. Tunajua uwezo mkubwa wa kushangilia wa mashabiki wetu na tunahitaji sapoti yao ili kutupa nguvu zaidi ya kupambana hadi dakika ya mwisho,” amesema Mohamed Hussein.