Hatimaye kile ambacho mashabiki wa Yanga SC walikuwa wakikisubiri kwa hamu kimetimia baada ya klabu hiyo kumtambulisha rasmi kiungo mkabaji wa kimataifa kutoka DR Congo, Fred Duval Ngoma, kama usajili mpya wa kuziba nafasi ya namba 6 ndani ya kikosi cha Wananchi.
Utambulisho huo ulifanywa na Rais wa Yanga SC, Hersi Said, huku ukihitimisha mjadala wa muda mrefu kuhusu mchezaji ambaye angeongeza nguvu eneo la kiungo cha ulinzi.
Ngoma, mwenye umri wa miaka 28, anatua Jangwani akitokea Olympique Club de Safi ya Morocco, ambako alikuwa na msimu mzuri na kuvutia kwa kiwango chake cha juu katika eneo la ukabaji na kuvunja mashambulizi ya wapinzani.

Kiungo huyo anatarajiwa kuongeza ushindani na uimara katika safu ya kati ya Yanga, eneo ambalo kwa misimu ya hivi karibuni limeongozwa vyema na Duke Abuya, Mudathir Yahya pamoja na Azizi Andambwile katika nyakati tofauti.
Mashabiki wa Yanga sasa wanatarajia kuona namna Fred Duval Ngoma atakavyoendana na mfumo wa timu hiyo huku akisaidia klabu kutimiza malengo yake ya kutwaa mataji ya ndani na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa msimu ujao.