Mpango wa Infantino wa Uwekezaji FIFA Wagonga Mwamba Baada ya Upinzani Mkali

Rais wa FIFA, Gianni Infantino, amepata pigo kubwa kisiasa baada ya mpango wake wa kuanzisha kampuni ya kibiashara ya kusimamia haki za mashindano ya FIFA, ikiwemo Kombe la Dunia, kushindikana kufuatia upinzani mkali kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka duniani.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, FIFA ilithibitisha kuwa imeondoa rasmi pendekezo hilo baada ya kuzua mgawanyiko mkubwa miongoni mwa mashirikisho ya soka na wadau wa mchezo huo.

Mpango huo ulikuwa unalenga kuanzisha kampuni mpya ya kibiashara ambayo asilimia 20 ya hisa zake zingeuzwa kwa wawekezaji binafsi, hatua iliyolenga kuongeza mapato na thamani ya biashara ya mashindano ya FIFA.

Hata hivyo, pendekezo hilo lilikumbana na upinzani mkali, huku UEFA ikitangaza kususia shughuli za FIFA hadi mpango huo ungeondolewa. Hatua hiyo ilionyesha wazi mgawanyiko uliokuwepo kuhusu mwelekeo wa uongozi wa FIFA chini ya Infantino.

Kwa kuwa mpango huo ulihusishwa moja kwa moja na Infantino, kufutwa kwake kunatazamwa kama pigo kubwa kwa uongozi wake, licha ya mafanikio makubwa ya kifedha ambayo FIFA imepata kupitia Kombe la Dunia lililomalizika hivi karibuni.

Mchambuzi wa uchumi wa michezo kutoka Chuo cha Holy Cross nchini Marekani, Victor Matheson, amesema kuwa wiki chache zilizopita Infantino alikuwa akionekana kuwa katika nafasi imara kutokana na mafanikio ya mapato yaliyotokana na Kombe la Dunia. Hata hivyo, amesema kushindwa kwa mpango huo kumetikisa hadhi yake kisiasa ndani ya FIFA na kumeibua maswali kuhusu mwelekeo wa uongozi wake katika siku zijazo.

Wachambuzi wanaamini uamuzi wa FIFA kuachana na pendekezo hilo unaonyesha nguvu ya mashirikisho wanachama na wadau wa soka katika kushawishi maamuzi makubwa yanayohusu mustakabali wa mchezo huo duniani.