Aliyekuwa mshambuliaji wa Young Africans SC, David Molinga maarufu kama ‘Falcao’, ameanza ukurasa mpya katika maisha yake ya soka baada ya kuteuliwa rasmi kuwa Rais wa Klabu ya AC Bandal kwa kipindi cha miaka mitano.
AC Bandal, yenye makao yake katika wilaya ya Bandalungwa jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ni klabu inayoshiriki Ligi ya EUFKIN-Malebo na pia ni timu ambayo Molinga aliwahi kuitumikia akiwa mchezaji kabla ya kuendelea na safari yake ya soka.
Baada ya kuthibitishwa katika nafasi hiyo, Molinga alitoa ujumbe wa shukrani akimshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hiyo na kueleza kuwa ni heshima kubwa kupewa jukumu la kuiongoza klabu hiyo, ambayo iliwahi kutwaa taji la Super Coupe ya Kinshasa mwaka 2014.
Aidha, aliwahakikishia wanachama, viongozi na mashabiki wa AC Bandal kuwa ataongoza kwa uwazi, uadilifu na kujituma ili kuhakikisha klabu hiyo inapiga hatua kubwa za maendeleo na mafanikio ndani na nje ya uwanja.
Uteuzi huo unamfanya David Molinga kuwa miongoni mwa wachezaji wa zamani wa Afrika waliofanikiwa kuingia kwenye nafasi za juu za uongozi wa vilabu baada ya kustaafu au kuelekea ukingoni mwa maisha yao ya soka.
Mashabiki wa soka nchini Tanzania bado wanamkumbuka Molinga kutokana na kipindi alichokitumikia Yanga, ambako aliwahi kuwa sehemu ya kikosi cha Wananchi katika Ligi Kuu Tanzania Bara.