Yanga Yamweka Depu Sokoni, Shalulile Atajwa Kuchukua Nafasi Yake

Tetesi za usajili zinaendelea kushika kasi zikidai kuwa Klabu ya Yanga inafikiria kumuuza mshambuliaji wake, Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’, katika dirisha hili kubwa la usajili ili kufungua nafasi ya kumsajili mshambuliaji mwingine mpya.

Kwa mujibu wa taarifa zinazosambaa, mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanatajwa kuwa kwenye mipango ya kumleta straika Peter Shalulile, jambo ambalo limeibua madai kuwa Depu anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji watakaoondoka ili kutoa nafasi katika kikosi.

Inaelezwa kuwa Depu bado ana mkataba wa miaka miwili na Yanga, baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na nusu alipojiunga na klabu hiyo mwezi Januari mwaka huu.

Licha ya tetesi hizo, mshambuliaji huyo bado yupo nchini Tanzania akiendelea na maandalizi ya msimu mpya pamoja na kikosi cha Yanga.

Hadi sasa, Yanga haijatoa tamko rasmi kuhusu hatma ya Depu, hivyo taarifa za kuondoka kwake zinaendelea kubaki katika kiwango cha tetesi za usajili hadi pale klabu au wahusika watakapotoa uthibitisho rasmi.