Kijana wa Mercedes, Kimi Antonelli, ameibuka mshindi wa mbio za Belgian Grand Prix na kuongeza pengo la uongozi katika msimamo wa madereva wa Formula One baada ya kutumia vyema bahati mbaya iliyompata mwenzake George Russell.
Ushindi huo wa Antonelli mwenye umri wa miaka 19 umehitimisha mbio tatu mfululizo bila ushindi na kumfanya afikishe tofauti ya alama 50 dhidi ya Russell, ambaye alilazimika kuachana na mbio mapema baada ya kugongana na bingwa mara saba wa dunia, Lewis Hamilton, kwenye mzunguko wa kwanza.
Akizungumza baada ya mbio, Antonelli alisema amefurahishwa kurejea kileleni baada ya kipindi kigumu.
“Inafurahisha sana kurudi kwenye ushindi baada ya mbio kadhaa ngumu. Ilikuwa mbio ngumu, tulipoteza uongozi wakati wa Virtual Safety Car lakini tulifanikiwa kuurudisha. Charles alikuwa na kasi kubwa hivyo ilibidi tupambane hadi mwisho,” alisema.
Charles Leclerc wa Ferrari alimaliza nafasi ya pili, huku bingwa mara nne wa dunia Max Verstappen wa Red Bull akimaliza wa tatu. Lewis Hamilton alimaliza wa nne licha ya kugongana na Russell mwanzoni mwa mbio, matokeo yaliyompa nafasi ya pili katika msimamo wa ubingwa akiwa nyuma ya Antonelli kwa alama 45.
Antonelli alikiri kuwa matokeo hayo yamechangiwa pia na bahati baada ya Russell kushindwa kumaliza mbio, akisema ni muhimu kutumia kila nafasi inayojitokeza katika vita vya ubingwa.
Kwa upande wake, Leclerc alisema aliamini angeweza kushinda hadi mizunguko ya mwisho, huku Verstappen akieleza kuwa yeye na Antonelli waliathiriwa na kipindi cha Virtual Safety Car, kilichozipa Ferrari nafasi ya kufanya mabadiliko ya matairi kwa faida kubwa.
Kwa ushindi huo, Antonelli ameimarisha nafasi yake kileleni mwa msimamo wa madereva huku mbio za kuwania ubingwa wa dunia wa Formula One zikiendelea kushika kasi.