HIZI HAPA REKODI ZA RAUNDI YA SABA LIGI YA WANAWAKE BONGO

LIGI ya Wanawake Tanzania kazi inaendelea kwa kila timu kuwa kwenye msako wa pointi tatu na kwenye raundi ya saba kuna maajabu saba yameandikwa tunakugusia baadhi namna hii:-

Mabao 12 yamefungwa kwenye mzunguko wa saba baada ya mechi tano kuchezwa ikionyesha ugumu wa ligi kuendelea tofauti na ilivyokuwa mzunguko wa sita yalipofungwa mabao 13.

Hakuna sare. Baada ya mechi zote tano kuchezwa hakuna timu iliyoambulia pointi moja. Ilikuwa ni lazima mtu apasuke na kuacha pointi tatu mazima tofauti na mzunguko wa sita ambapo zilikusanywa sare mbili, Bunda 0-0 Simba Queens na Geita Gold Queens 2-2 Fountain Gate Princess.

Timu iliyofungwa haijafunga. Kazi kubwa ilikuwa kwa timu itakayofungwa ilikwama kupata nafasi ya kuwafunga wapinzani wao hivyo timu zote zilizoambulia ushindi makipa wao walitoka na hati safi ndani ya dakika 90.

Nyumbani kapoteza mmoja. Kwenye mzunguko wa saba ni Fountain Gate Princess pekee ilipoteza ikiwa nyumbani Uwanja wa Jamhuri Dodoma ilivyopasuliwa na JKT Queens bao 1-0 na kuacha pointi tatu mazima. Raundi ya pili ni timu mbili zilipoteza nyumbani Yanga Princess 1-3 JKT Queens, Alliance Girls 1-2 Baobab Queens.

Nne zatamba nyumbani, timu nne zilizokuwa nyumbani zilitumia vema faida ya kuwa nyumbani kwa kupata ushindi kwenye mechi zao. Ilikuwa ni Yanga Princess 1-0 Bunda, Simba Queens 7-0 Alliance Girls, Ceasiaa Queens 2-0 Baobab Queens, Amani Queens 1-0 Geita Gold Queens.

Hat trick Azam Complex. Kwenye raundi ya saba hat trick moja ilipatikana Uwanja wa Azam Complex kupitia kwa nyota wa Simba Queens Jentrix Shikangwa.

Simba na JKT Queens hazijapoteza. Mpaka raundi ya saba inachezwa wababe wawili hawajaonja joto ya kuyeyusha pointi tatu uwanjani ambao ni Simba Queens na JKT Tanzania.

Imeandikwa na Dizo Click na kutoka gazeti la Championi Jumatano.