Home Sports BURUDANI SAWA, MANDONGA UTANI WAKE USIVUKE MIPAKA

BURUDANI SAWA, MANDONGA UTANI WAKE USIVUKE MIPAKA

KARIM Mandonga ni sawa na kachumbari ya mchezo wa ngumi kipindi hiki, hili halina ubishi.

Mandonga sasa ni gumzo haswa, kama mtu ni mgeni, anaweza kuamini Mandonga ni bondia mwenye mikanda kadha wa kadha kutokana na ubora wa kazi yake ulingoni.

Bondia huyu si maarufu kutokana na ushindi ulingoni, amepata bahati ya aina yake kuwa ni bondia maarufu kwa kupigwa.

Kwa kifupi sasa Mandonga ni ‘brand’ (Nembo) ambayo inatokana na aina yake, kwamba kupoteza kwake si jambo la kujutia.

Wakati mwingine, Mandonga amesikika akijivunia namna anavyoweza kupoteza michezo yake na baadaye akajivunia namna anavyoweza kuendelea kuwa maarufu licha ya vipigo.

Ukimuangalia ni mtu asiye na hofu na kupoteza jambo badala yake amekuwa burudani kutokana na Maisha aliyochagua.

Kutokana na uchale wake, Mandonga amechagua kuwa kivutio hasi na si chanya. Naweza sema si jambo baya sana pale watu wanapoamua kuburudika kwa aina nyingine na si kwenda mbele kwa maana ya chanya.

Sote tunafahamu kwamba mafanikio ni mambo kuwa chanya, kwamba unaongeza kitu kwa maana ya kupata na si sherehe ya kukosa.

Umaarufu wa Mandonga, unamsaidia kuendeleza maisha yake kwa kuwa watu wamechagua namna hiyo lakini bado lazima tuwe makini na kulinda mambo kadhaa muhimu katika mchezo wa ngumi ambao kwa sasa umaarufu wake unaendelea kupaa kwa kasi.

Lazima tuangalie heshima yake lakini pia tuangalia mwendo wa vizazi vijavyo. Yes, Mandonga yupo kama sehemu ya burudani lakini isichukue nafasi kubwa kupitiliza hadi kufikia kuwaaminisha vijana wetu kwamba mtu anayepigwa kila wakati ndiye shujaa.

Tusifanye ikafikia kizazi kijacho cha mchezo wa ngumi kikaanza kuamini kwamba anachofanya Mandonga ndicho sahihi zaidi kuliko na huenda watakapokua wanaweza kuwa kama yeye.

Hii ni tahadhali, kwangu naamini taifa halihitaji Mandonga mwingine kwa kuwa mchezo wa ngumi ni hatua. Kuwa na bondia anayefanya vizuri nyumbani na nje ya hapa huku akifanikiwa kubeba mikanda.

Achana na hivyo, angalia Mandonga amekuwa wakati mwingine akipata huduma bora zaidi kuliko hata mabondia wanaofanya vizuri.

Maana yake kufanya vizuri hakuna maana kuliko anayepoteza. Inawezekana haya yakawa hayaonekani sasa lakini ni mambo ambayo yanapaswa kupimwa na lazima tukubaliane kwamba anayefanya vizuri, ndiye anayepaswa kulipwa vizuri.

Hata Mandonga, anapaswa kufanya vema zaidi ili apate mapambano zaidi yatakayomlipa zaidi.Akiendelea hivi, watu watamchoka.

Mwisho ni heshima kwa mchezo wa ngumi, tumeona pambano la Mandonga na Said limefutwa juzi kutokana na mwamuzi kutofanya kazi yake vizuri. Kwanini alifnya hivyo? Sote tumeona alikuwa akijaribu kumlinda Mandonga ambaye hakuwa makini.

Mandonga hajutii kupoteza au kufanya vibaya, utani ulikuwa mwingi hadi unaondoa ladha ya mchezo wa ngumi na bahati mbaya mwamuzi alitumia nguvu nyingi kumlinda na mwisho ukawa uamuzi wa kulifuta pambano ili kufuta aibu inayoufanya mchezo wa ngumi ni wa kuchezeachezea au kufanyia utani.

Utani wa Mandonga, unaanza kuingia kwa waamuzi, hatari siku ukiingia kwa viongozi wa mchezo wenyewe na mwisho tutajisahau na kuufanya mchezo wa ngumi kuwa wa vichekesho, tutapotea.

Kuna nguvu ya watu wengi wanaowekeza nguvu kwenye mchezo huo na kuufanya urejee tena kwa maana ya kukua. Kama utani wa aina hii utachukua nguvu kupita kiasi, tutawakatisha tamaa na ikiwezekana kutakuwa na ugumu kuwarudisha mara nyingine.

Kuburudika, naungana nanyi lakini msisitizo wangu lazima kuwe na mipaka. Burudani ya mchezo huu ni ubora wa masumbwi na mapambano bora na vichekesho vilivyopitiliza.

Kama kuna vichekesho, basi viwe na nafasi yake ndogo na kuvifanya viwe vina nafasi kubwa kuliko ubora wa mchezo wenyewe kwa kuwa,kila tulipo tunapaswa kupiga hatua na kama tunajitambua, kamwe mchezo wa ngumi hauwezi kupiga hatua kwa vichekesho na utani wa nundu za Mandonga.

Previous articleSHABIKI WA SIMBA ASHINDA MILIONI 49 NA10 BET
Next articleUSHINDI UWE NA MWENDELEZO KIMATAIFA KWA TIMU ZA TAIFA