Home Uncategorized YANGA YAICHAPA KWA MARA NYINGINE AZAM FC KWAO

YANGA YAICHAPA KWA MARA NYINGINE AZAM FC KWAO

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wameituliza kwa mara nyingine tena Azam FC baada ya kuwatungua mabao 2-1 kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC ni wao walianza kupata bao la kuongoza kupitia kwa Rodgers Kola ilikuwa dk ya 10 liliwekwa usawa na Djuma Shaban kwa mkwaju wa penalti dk ya 17 na kuwafanya warudi mchezo kwa kasi ileile.

Kipindi cha kwanza kilikamilika kwa timu hizo kutoshana nguvu ila kipindi cha pili mambo yalikwenda tofauti kwa mashabiki wa Azam FC ambao walikuwa nyumbani.

Bao la ushindi lilifungwa na Fiston Mayele ambaye alifikisha jumla ya mabao 11 kwenye ligi akiwa ni namba moja kwa watupiaji kwa msimu wa 2021/22 anafuatiwa na Relliats Lusajo mwenye mabao 10 yeye anakipiga Namungo FC.

Yanga inajikita nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 51 baada ya kucheza mechi 19 na bado haijapoteza mchezo hata mmoja kwenye ligi.

Mchezo wa kwanza walipokutana Uwanja wa Mkapa ubao ulisoma Yanga 2-0 Azam FC hivyo kwenye mchezo uliochezwa usiku wa kuamkia leo Azam FC imekwama kutamba ikiwa nyumbani.

Kocha Mkuu wa Azam FC,Abdihamid Moallin amesema kuwa anafikiria ulikuwa ni mchezo wa timu zote lakini bahati ilikuwa ni upande wa Yanga.

“Tulijitahidi kuweza kuanza kufanya vizuri kwenye umiliki lakini haikuwa hivyo kwetu, unajua Yanga ni timu kubwa hivyo iliweza kutumia makosa ambayo tulifanya,” amesema.

Previous articleMUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA ALHAMISI
Next articleSIMBA KAZINI LEO MBELE YA COASTAL UNION,MKWAKWANI