Man United na Arsenal Zapigania Saini ya Tonali

Vilabu vya Manchester United na Arsenal FC vinatajwa kuingia kwenye vita ya kuwania saini ya kiungo wa Newcastle United, Sandro Tonali, katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, klabu zote mbili zimeonyesha nia ya kumtaka nyota huyo wa Italia, ambaye anatarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuondoka Newcastle mwishoni mwa msimu huu.

Mwandishi maarufu wa usajili, Fabrizio Romano, ameripoti kuwa Tonali hana mpango wa kurejea Serie A, badala yake analenga kuendelea kucheza soka nchini England msimu ujao.

Hali ya Newcastle kwenye msimamo wa Premier League wakiwa nafasi ya 14 huku wakiwa bado hawajajiwekea uhakika wa kubaki ligi kuu inaelezwa kuwa moja ya sababu inayoweza kuchangia kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wake muhimu.

Tonali, aliyesajiliwa kutoka AC Milan mwaka 2023 kwa ada ya pauni milioni 55, anaripotiwa kuwa anaweza kuuzwa kwa ada inayokaribia mara mbili ya hiyo.