MASHUJAA FC vs Yanga SC ni mchezo unaofuata kwenye ratiba ya NBC Premier League Juni 13, 2026 huku benchi la ufundi la mabingwa watetezi likibainisha kwamba lipo tayari kwa mchezo.
Ahamid Moallin, Kocha Mkuu wa Yanga SC amesema wanatambua ushindani uliopo watapambana kupata matokeo mazuri uwanjani.
“Hakuna mchezo rahisi katika ligi hii. Haijalishi tunacheza na timu ya mwisho kwenye msimamo au timu ya pili, kila mchezo kwetu ni fainali. Lengo letu ni kutwaa ubingwa wa tano na kila mchezo ni hatua muhimu kuelekea kufanikisha azma hiyo.
“Iwapo tutashinda kwa mabao mengi au machache si jambo la msingi. Kilicho muhimu ni kupata ushindi na alama tatu.
“Wachezaji wetu ni wenye uzoefu mkubwa lakini pia ni wanyenyekevu sana. Licha ya mambo mbalimbali yanayosemwa nje ya uwanja, wao wamebaki wakifanya kazi kwa bidii kila siku. Wengine wanapigania ubingwa wao wa tano, wengine wa pili na wengine wa kwanza, lakini wote wana njaa ya kumaliza msimu huu kwa nguvu,”.