Home Sports SAKHO,BANDA WAMPA KIBURI PABLO KIMATAIFA

SAKHO,BANDA WAMPA KIBURI PABLO KIMATAIFA

KUREJEA kwa Pape Ousmane Sakho ambaye aliumia katika mchezo dhidi ya ASEC Mimosas na kuimarika kwa kiwango cha winga Peter Banda, kumempa kiburi Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco kufanya vizuri katika mchezo wa leo Jumapili dhidi ya Union Sportive Gendarmerie Nationale ya nchini Niger.

Simba leo Jumapili wanatarajiwa kumenyana na Union Sportive Gendarmerie Nationale katika mchezo wa pili wa
Kundi D ndani ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa kwenye Dimba la Général Seyni Kountché lililopo Niamey, Niger.

Katika hatua ya makundi, Simba imeanza vizuri ikishinda mchezo wa kwanza nyumbani kwa mabao 3-1 dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.

Kwa upande wa wapinzani wao wa leo, walipoteza mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya RS Berkane ya nchini Morocco kwa kufungwa mabao 5-3.

Pablo ameweka wazi kuwa, Sakho tayari yupo fiti baada ya kukosekana katika mchezo uliopita wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Ruvu Shooting, huku akifurahishwa na baadhi ya wachezaji wake ambao viwango vyao vimezidi kuimarika akiwemo Banda na Israel Patrick Mwenda.

“Sakho yupo fiti kwa sasa, tuliona ni vema kumpumzisha katika mchezo dhidi ya Ruvu, lakini yupo vizuri kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Union Sportive Gerndamarie.

“Wachezaji wapo tayari kwa mechi na habari njema ni kwamba wachezaji wengi wameonekana kuimarika
tofauti na awali. Peter Banda na Israel Mwenda ni mfano katika hili, wengine pia wanafanya vizuri,naamini watakuwa msaada kwetu kwa ajili ya kufanya vizuri katika mchezo huu,” amesema kocha huyo

Previous articleNYOTA 7 YANGA WATIBUA MIPANGO YA KOCHA NABI
Next articleAZAM FC BADO HAIJAFIKA KWENYE UBORA WENYEWE