HONGERA Kwa timu ambazo zimeweza kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Mapinduzi na kesho wanatarajiwa kuweza kucheza na kumpata mshindi.
Ipo wazi kwamba kila timu inahitaji ushindi na ambaye atajipanga ana nafasi kubwa ya kuweza kutwaa Kombe la Mapinduzi ambalo ni heshima na litawafanya mashabiki aweze kufurahi.
Mabingwa watetezi wao wamefungashiwa virago ambao ni Yanga kwa kutolewa kwao basi zile lawama kwamba fulani amemkimbia fulani hazina maana bali itazamwe namna ambayo itawafanya wazidi kuwa imara.
Kupambana na kufika hatua ya nusu fainali haina maana kwamba ilikuwa ni bahati mbaya na wangekimbia kufika hatua ya fainali hapana hilo sio kweli na haiwezekani timu ipambane ikiwa na hofu ya kufika hatua ya fainali.
Jambo la msingi ni kukubali matokeo kwa kuwa yameshatokea na huwezi kuyabadili kwa namna yoyote ile itakuwa hivyo na imeshakuwa.
Kikubwa ambacho kinatakiwa kwa sasa mashabiki wa Yanga pamoja na timu nyingine ambazo zimeshindwa kutinga hatua ya fainali ni kuanza mipango kazi upya kwa ajili ya wakati ujao.
Tunaona kwamba timu za Zanzibar zimeishia katika hatua ya makundi kwenye hili pia ni muhimu kwa timu kuanza mipango kwa ajili ya wakati ujao.
Itakuwa nzuri fainali ikiwa inazikutanisha timu zote za kila pande iwe ni kutoka bara na visiwani hapo itakuwa na ile ladha ya ushindani wa kweli.
Lakini kwa kuwa makosa ambayo yametokea makocha wameona imani yangu watayafanyia kazi ili wakati mwingine kuwe na utofauti kwenye fainali.
Yote kwa yote pongezi kwa KMKM, Mlandege, Meli 4 FC,Yanga kwa namna ambavyo zimeweza kuonyesha ushindani bila kuisahau Selem View na timu zote ambazo zilishiriki.
Kuelekea kwenye fainali ya kesho ambayo itawakutanisha Azam FC v Simba muhimu sana kwa wachezaji kucheza mchezo wa kiungwana.
Kwa Simba sina mashaka nao hasa kwa kucheza kwa tahadhari kubwa na kupenda mpira wa pasi licha ya kwamba wapo wachezaji ambao wamekuwa na hasira za haraka ikiwa ni pamoja na beki Henock Inonga.
Pia kiungo Bernard Morrison na beki Pascal Wawa ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa na rekodi za kuwa kwenye matukio ya kutumia nguvu nyingi.
Azam FC ikiwa watacheza lile soka la kutulia itakuwa sawa lakini zile faulo ambazo huwa anapenda kuzicheza Frank Domayo lazima zisipewe nafasi kwa kuwa itakuwa rahisi kwa wachezaji kuumizana.
Pia Ibrahim Ajibu ambaye ni kiungo ameonekana kuwa na mtindo wa kucheza faulo pale anapokuwa na mpira hilo nalo lisipewe nafasi, migongano ipo lakini fainali lazima iheshimiwe na uchezwe ule mpira mkubwa.
Kwa sasa kuongeza idadi ya mejeruhi kwenye timu moja ni hasara kubwa na mlinzi wa mchezaji ni mchezaji mwenyewe. Kila la kheri kwenye maandalizi ya mwisho na mshindi ni yule ambaye atakuwa amefanya maandalizi mazuri.
Ubabe tupa kule mpira uchezwe kwa amani na upendo kwani maisha ya mchezaji yanategemea mpira.