IMEELEZWA kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Mhispania, Franco Pablo, muda wowote atawaambia mabosi wa timu hiyo wampe mkataba kiungo mkabaji Mnigeria, Udoh Etop David.
Mingeria huyo yupo Unguja, Zanzibar akiendelea na majaribio ya timu hiyo iliyopo katika michuano ya Kombe la Kagame.
Wachezaji wengine waliopo katika majaribio hayo ni Muivory Coast, Chekhi Moukoro na Msudan, Sharraf Shiboub ambaye aliwahi kuichezea timu hiyo.
Mmoja wa mabosi wa timu hiyo, amesema kocha amefurahishwa na kiwango cha kiungo huyo mwenye umbile kubwa anayetumia miguu yote.
Bosi huyo alisema kuwa Pablo amempa mchezo mmoja wa Kombe la Mapinduzi kwa ajili ya kumuangalia zaidi kiungo huyo ambaye ni mtulivu akiwa na mpira.
Aliongeza kuwa kocha huyo hajaridhishwa na kiwango cha Moukoro na Shiboub ambao muda wowote wataondelewa katika kambi ya timu hiyo iliyokuwepo Zanzibar.
“Tumebakiza nafasi moja ya kusajili mchezaji wa kimataifa na Moukoro, Shiboub na Etop ndiyo wanaoiwania nafasi hiyo.
“Kocha anadai hajaridhishwa na kiwango cha nyota wawili Shiboub na Moukoro huku akiomba kumtazama zaidi Etop.
“Hivyo upo uwezekano mkubwa wa Etop kusajiliwa katika dirisha hili dogo baada ya kuonekana ana kiwango kikubwa cha kucheza nafasi hiyo ya kiungo,” alisema bosi huyo.
Pablo alizungumzia hilo na kusema kuwa: “Naendelea kuwaangalia Shiboub, Etop na Moukoro na mmoja wapo ndiye nitakayepitisha usajili wake, hivyo nitaendelea kuwaangalia zaidi katika michezo ijayo ya Kombe la Mapinduzi.”