SIMBA SC V AZAM FC MWENDO WA HESHIMA, AJIBU OUT

PABLO Franco, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa anawaheshimu wapinzani wake Azam FC ambao atakutana nao Uwanja wa Mkapa leo Januari Mosi, 2022 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

 

Huu ni mchezo wa kwanza kwa vigogo hawa kukutana msimu wa 2021/22 na unapigwa siku ya kwanza ya mwaka 2022.


Akizungumza mbele
ya Waandishi wa Habari, Pablo alisena kuwa anawatambua vyema Azam FC na ni timu yenye
wachezaji wazuri wenye
uwezo mkubwa.


“Nawaheshimu Azam FC
ni timu nzuri na wachezaji wake pia ni wazuri niliweza kuwafuatilia na kuona walivyocheza katika mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting, walicheza vizuri na niliona mchezaji wao mmoja anaitwa Kangwa (Bruce) alihusika kwenye mabao mengi.


“Mashabiki wajitokeze
kwa wingi kutakuwa na burudani pia hasa ukizingatia ni mwaka mpya 2022 nawatakia kheri. Kuwepo kwa Ajibu (Ibrahim) ama asiwepo hilo litakuwa juu ya benchi lao la ufundi lakini ninachojua Ajibu ni mchezaji mzuri lakini alikosa nafasi,” alisema.


Kwa upande wa Idd
Aboubakhari, Kocha wa Makipa wa Azam FC alisema kuwa wanatambua Simba
ni timu kubwa na
wanawaheshimu ila wanahitaji pointi tatu.


“Simba ni timu kubwa
na ina wachezaji wazuri, tumetazama mechi zao na ninatambua kwamba wao watakuwa
wametufuatilia, dakika
15 za mchezo itakuwa ni kwa ajili ya kusoma mbinu za wapinzani wetu kisha
tutajua nini tutafanya.


“Ujio wa Ajibu ni
mipango ya benchi lakini kusema kwamba anaweza kuanza itakuwa ngumu kwani mipango ya timu huanza muda mrefu ikiwa tutamchezesha labda inaweza kuwa sapraizi.


“Kuhusu kutokuwepo
kwa Never Tigere, Prince Dube ambao wapo kwenye timu ya taifa sio tatizo kwani tuna wachezaji 30 na hao tunawaombea kheri,” alisema. Nahodha wa Azam FC, Sospeter Bajana alisema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo.

STORI: LUNYAMADZO MLYUKA NA REHEMA NASSORO