PILATO wa mchezo wa Desemba 11 ambao ni mchezo wa Kariakoo Dabi kati ya Simba v Yanga ni kiboko kwa kuwa kwenye mechi zote ambazo alihusika kwenye orodha ya waamuzi ilikuwa ni lazima jitu lipasuke.
Kwa msimu wa 2021/22, Elly Sasii ambaye ameteuliwa kuwa mwamuzi wa kati ameweza kuwa kwenye orodha za waamuzi katika mechi nne ambazo ziliwahusu Simba v Yanga.
Kwenye mechi hizo moja ilikuwa ni ile ya ufunguzi wa ligi ambapo alishuhudia jitu likipasuka kwa kupigwa bao 1-0 na ni mechi moja tu aliweza kusimamia iliyowahusu Yanga ambapo alikuwa mwamuzi wa kati na alishuhudia Azam FC ikiambulia kichapo.
Pia suala la kadi kwake ni utalii tu kwa kuwa aliwahi kushuhudia wachezaji wakionyeshwa kadi nyekundu pamoja na njano za kutosha lakini hakuwa na bahati kushuhudia mkwaju wa penalti.
Rekodi zake zipo namna hii:-Septemba 25,2021 alikuwa ni mwamuzi wa akiba katika mchezo wa Kariakoo Dabi ambapo baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 0-1 Yanga mwamuzi wa kati kwenye mchezo huo alikuwa ni Ramadhan Kayoko.
Kayoko kwenye mchezo huo alionyesha jumla ya kadi 8 za njano na moja ilikuwa nyekundu kwa Taddeo Lwanga wa Simba ambaye alionyeshwa kadi mbili za njano.
Oktoba 2, alikuwa mwamuzi wa akiba ambapo alishuhudia ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Yanga 1-0 Geita Gold, mwamuzi wa kati ambaye alikuwa ni Ahmed Arajiga alitoa jumla ya kadi nne za njano.
Oktoba 30 alikuwa ni mwamuzi wa kati na ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Yanga 2-0 Azam FC ambapo aliweza kumuonyesha kadi ya njano Khalid Aucho.
Novemba 3, Uwanja wa Mkapa alikuwa ni mwamuzi wa akiba wakati Simba iliposhinda bao 1-0 dhidi ya Namungo kwenye mchezo huo mwamuzi wa kati alikuwa ni Nassoro Mwichui aliweza kumuonyesha kadi nyekundu ya moja kwa moja Abdulaziz Makame.