MBWANA MAKATA ANATAMBA NDANI YA TATU BORA

MBWANA Makata ni kocha mzawa pekee ambaye yupo ndani ya tatu bora kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2021/22.

Akiwa ndani ya Dodoma Jiji, Makata amekuwa kwenye mwendo bora ambapo mpaka sasa amekuwa akigawa zabibu kwenye mechi zake ambazo wanacheza na wachezaji wake wengi asilimia mia ni wazawa.

Kikosi hicho baada ya kucheza mechi saba kimekusanya jumla ya pointi 12 kibindoni.

Ni mabao matano ambayo wamefunga washambuliaji wake na wamepoteza mchezo mmoja pekee kati ya mechi 7 kwa msimu huu mpya.

Nafasi ya kwanza ipo mbele ya Yanga ambao wao wamekusanya pointi 19 na wananolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi raia wa Tunissia.

Nafasi ya pili ipo mikononi mwa Simba ambao wana pointi 14 wakiwa wamecheza mechi sita na leo wana kazi ya kusaka ushindi mbele ya Geita Gold, Uwanja wa Mkapa.

Simba inanolewa na Kocha Mkuu, Pablo Franco ambaye ni raia wa Hispania.

Mchezo ujao kwa Dodoma Jiji ni dhidi ya Mbeya City na unatarajiwa kuchezwa Desemba 6, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Makata amesema kuwa wachezaji wamekuwa wakifuata maelekezo na kufanya kazi kwa jitihada bila kukata tamaa.