>

STERLING KUSAINI DILI JIPYA CITY

MANCHESTER City wana imani kubwa ya kumpa dili jipya nyota wao Raheem Sterling ili aweze kuendelea kuitumikia timu hiyo kwa kuwa dili lake linakaribia kumeguka na yeye ameanza kuwa kwenye ubora.

Kiungo huyo alianza msimu wa 2021/22 vibaya ambapo aliweza kucheza mechi nne kisha akaweka wazi kwamba anahitaji kuondoka ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Pep Guardiola.

Nyota huyo mwenye miaka 26 kwa sasa amerejea kwenye ubora wake baada ya kufunga kwenye ushindi dhidi ya Club Brugge,Everon na Paris Saint Germain, (PSG) ikiwa ni mara ya kwanza tangu Agosti 2020 ambapo aliweza kufunga kwenye mechi tatu mfululizo.

Mkataba wake umebakiza miezi 18 ili kuweza kukamilika kwenye kikosi hicho na imeripotiwa kwamba mabosi wake City wana imani kwamba atasaini dili jipya kwa kuwa awali alikuwa anahitaji kupata uhakika kwamba yeye ni chaguo la kwanza kwa kocha Guardiola.

Jambo lingine ambalo linamfanya nyota huyo aweze kupata nafasi ni pamoja na kuumia kwa kiungo aliyekuwa akianza kikosi cha kwanza Jack Grealish ambaye mara nyingi amekuwa akicheza upande wa kushoto.