KOEMAN APEWA MKONO WA KWAHERI BARCELONA

RONALD Koeman amefutwa kazi jumlajumla ndani ya kikosi cha Barcelona kinachoshiriki La Liga nchini Hispania ikiwa ni baada ya miezi 14 kutumia katika kutimiza majukumu yake ndani ya timu hiyo huku jina la Roberto Martinez likitajwa kurithi mikoba yake.

Kwa msimu wa 2021/22 ndani ya La Liga, Koeman alikiongoza kikosi chake kushinda mechi 10 na alipokea mikoba ya Quique Setien ndani ya Nou Camp ilikuwa Agosti 2020 na alifanikiwa kushinda taji ka Copa del Rey katika msimu wake wa kwanza.

Kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Rayo Vallecano ndani ya La Liga mchezo uliochezwa Oktoba 27 na bao likipachikwa na Radamel Falcao dakika ya 30 ulikuwa ni mchezo wake wa mwisho kukaa benchi na ulifanya awe amefungwa jumla ya mechi sita katika mashindano yote.

Maelezo ambayo yalithibitishwa na Rais wa Barcelona Joan Laporta yalieleza kuwa ni kweli Koeman hatakuwa na majukumu ndani ya Barcelona iliyo nafasi ya 9 na pointi 15 baada ya kucheza mechi 10 kwenye La Liga na atawaaga wachezaji wa timu hiyo leo Alhamisi kwa kuwaambia kwaheri.

Ripoti zinaeleza kuwa miongoni mwa wanaoweza kurithi mikoba yake ni pamoja na kiungo wa zamani wa timu hiyo Xavi, Roberto Martinez kocha wa Ubelgiji pamoja na River Plate kocha Marcelo Gallardo.