OKTOBA 23, Mason Mount nyota wa Chelsea mwenye miaka 22 aliandika rekodi yake tamu kwa kufunga hat trick mbele ya Norwich kwenye mchezo wa Ligi Kuu England jambo ambalo lilimpa tabasamu nyota huyo ambaye yupo chini ya Kocha Mkuu, Thomas Tuchel.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu England, ubao wa Uwanja wa Stamford Bridge ulisoma Chelsea 7-0 Norwich huku Mount akitupia mabao matatu yeye mwenyewe.
Ikumbukwe kwamba nyota huyo alikuwa ameweka rekodi mbovu ya kucheza jumla ya mechi 25 bila kufunga kwenye timu yake hiyo pamoja na timu ya taifa ya England.
Nyota huyo amesema:”Kabla ya mechi nilijiambia mwenyewe kwamba ni lazima nifunge, halafu mabao matatu yakaja kwenye mchezo mmoja, ni tukio kubwa ambalo nitalikumbuka kwa kweli.
“Nimekuwa nikisubiri kwa muda mrefu, nilikuwa najiweka katika nafasi ya kufunga lakini sikuwa naweka mpira kwenye nyavu kwangu mimi ilikuwa ni tukio kubwa kufunga mabao matatu kwenye Uwanja wa Stamford Bridge ilikuwa ni kitu maalumu sana,”