>

SALAH NI MZEE WA MAREKODI TU MAJUU

MOHAMED Salah, nyota anayekipiga ndani ya Liverpool inayonolewa na Kocha Mkuu, Jurgen Klopp amekuwa na wakati mzuri kwa msimu huu wa 2021/22 akiendelea kuandika rekodi matata kila iitwapo leo.

Raia huyo wa Misri anatajwa kuwa mchezaji bora duniani kwa zama za wakati huu na ni tegemeo pia kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Misri hivyo ninja bado anaaminika kila kona.

Akiwa anacheza ndani ya Ligi Kuu England mwamba huyo amefanikiwa kuandika rekodi matata ambazo kwa sasa zimekuwa wimbo wa wengi wanaomfuatilia hasa mashabiki wake kutoka Afrika bila kusahau dunia nzima kiujumla.

Nyota huyo ameweka rekodi ya kuwa raia wa kwanza kutoka bara la Afrika kutupia mabao 106 kwenye historia ya wachezaji kutoka bara la Afrika ambao wamecheza Ligi Kuu England jambo ambalo linahitaji ujasiri na juhudi isiyo ya kawaida.

Salah ameweza kuivunjavunja rekodi ya Legend, raia wa Ivory Coast wakumita Didier Drogba ambaye yeye alipokuwa akitumika ndani ya Ligi Kuu England alitupia jumla ya mabao 104 hivyo ninja kamzidi mabao mawili na bado anapewa nafasi ya kufunga zaidi kwa sababu bado Salah anacheza huku Drogba akiwa ameshatundika daruga.

Pia Salah amefanikiwa kuwa mchezaji ambaye ameweza kupiga hat trick ndani ya Uwanja wa Old Trafford ikiwa imeyeyuka miaka 18 ambapo aliyefanya hivyo alikuwa ni Cristiano Ronaldo ambaye kwa sasa anakipiga ndani ya Manchester United.

Kwenye historia ya maisha ya soka la Liverpool Salah amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao mfululizo bila kukoma kwenye mechi 10 na hiyo amefanya kwenye michuano yote jamaa kila mechi ambayo alikuwa anaanza ilikuwa ni uhakika kufunga.

Ukiweka kando rekodi hiyo Salah amekuwa ni mchezaji wa kwanza kufunga katika mechi tano mfululizo ugenini na mtu wa mwisho kuweka rekodi hiyo ilikuwa ni mwaka 1902 ila ni ndani ya Liverpool.