PROFESA JAY: UNAFIKI HAUTUSAIDII JAMBO LOLOTE LILE

MKONGWE wa muziki wa Bongo Fleva, Joseph Leonard Haule ‘Profesa Jay’ anasema kuwa, wasanii wanatakiwa kupendana na kuacha tabia za kinafiki kwa sababu wakiendekeza tabia hizo hazitaufikisha muziki wao pale wanapopataka.

Jay ambaye mpaka sasa bado anakimbiza na ngoma yake kali ya Utaniambia Nini anasema kuwa, kuna baadhi ya wasanii hawapendani kabisa; yaani wanashindwa hata kusapotiana vizuri kwenye kazi jambo ambalo siyo zuri na halimfurahishi.

“Sijui ni kwa nini wasanii siku hizi hawapendani; yaani wamejawa na tabia za kinafki, wanashindwa hata kusapotiana kwa sababu ya kuoneana wivu, binafsi sipendi kabisa tabia ya namna hiyo kwa sababu inarudisha gemu ya muziki wetu nyuma na itakuwa ngumu sana kujulikana kimataifa kwa sababu wenyewe kwa wenyewe hatupendani,” anasema mkongwe Profesa Jay.