>

SIMBA MATUMAINI MAKUBWA NDANI YA LIGI KUU BARA

KOCHA msaidizi wa Simba, Hitimana Thiery amesema kuwa watarudi kwa nguvu zote kuhakikisha kuwa wanafanya vizuri katika michezo ya ligi kuu mara baada ya kumaliza ratiba yao ya michuano ya ligi ya Mabingwa.

Simba mpaka sasa katika michezo ya ligi kuu imefanikiwa kucheza michezo miwili pekee dhidi ya Biashara United na Dodoma Jiji ambapo wamefanikiwa kushinda katika mchezo mmoja na kutoa sare mmoja jumla wakiwa na pointi 4.

Hitimana Thiery amesema kuwa watu wasifikiri kuwa wamewekeza nguvu katika michuano ya kimataifa pekee kwani malengo yao ni kuhakikisha wanafanya vyema katika kila michuano wanayoshirki na baada ya kumaliza kwa ratiba ya michuano hiyo wataelekeza nguvu zote katika michezo ya ligi kuu.

“Kila michuano ambayo Simba inashiriki malengo ni kufanya vizuri, hivyo watu wasifikiri kuwa labda tumewekeza nguvu katika michuano ya kimataifa pekee hapana hata kwenye michezo ya ligi kuu tutahakikisha kuwa tunafanya vizuri.

“Malengo ya Simba katika ligi kuu yapo wazi ni kuhakikisha kuwa tunatetea ubingwa ambao tuliweza kuubeba msimu uliopita, hivyo tutarejea kwa kishindo na kufanya vizuri katika michezo yetu ijayo ya ligi ili tuweze kuendelea kufanya vizuri na kuwa ndani ya malengo yetu ambayo hayawezi kutimia kama hatushindi,”alisema kocha huyo.

Kwa sasa mambo ni magumu ndani ya Simba baada ya kunyooshwa kwa mabao 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Uwanja wa Mkapa na kuweza kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo kwa sasa itashiriki Kombe la Shirikisho.

Mchezo wao ujao kwenye ligi ni dhidi ya Polisi Tanzania unaotarajiwa kuchezwa kesho Oktoba 27, Uwanja wa Mkapa.